WAZIRI MKUU MHE:PINDA ASISITIZA UWAZI KATIKA MATUMIZI YA TAKWIMU SAHIHI

2
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akionyesha kitabu kinachoeleza Maendeleo na historia ya Takwimu katika Bara la Afrika alichokizindua leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu (ISI) Bw. Vijay Nair na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
4
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akizindua kitabu kinachoeleza Maendeleo na historia ya Takwimu katika Bara la Afrika alichokizindua leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu (ISI) Bw. Vijay Nair na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kushoto kwa Waziri Mkuu na Prof. Ben Kiregyeza (kulia) ambaye ndiye mwandishi wa kitabu hicho.
5
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akifungua  Kongamano la Kimataifa la Siku 3 la Wakuu wa Taasisi za Takwimu wa nchi 38 za Afrika na 18 kutoka nje ya Bara la Afrika leo jijini Dar es salaam.
6
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa awali akizungumza na Wakuu wa Taasisi za Takwimu wa nchi 38 za Afrika na 18 kutoka nje ya Bara la Afrika waliohudhuria Kongamano la Siku 3 la Kimataifa kujadili Matumizi ya Takwimu leo jijini Dar es salaam.
7
Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu (ISI) Bw. Vijay Nair akizungumza kabla ya uzinduzi wa  Kongamano  la Kimataifa la masuala ya Takwimu la Wakuu wa Taasisi za Takwimu wa  kutoka Afrika na nje ya Afrika.
8
Waziri Mkuu akizungumza jambo na Makamu wa Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu (ISI) Bi. Irena Krizman leo jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua  kongamano la Wakuu wa Taasisi za Takwimu wa nchi 38 za Afrika na 18 kutoka nje ya Bara la Afrika. Katikati ni mjumbe kutoka ya Kusini Bw. Pali Lihohla.
9
Waziri Mkuu akizungumza akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua  kongamano la Wakuu wa Taasisi za Takwimu wa nchi 32 za Afrika na 18 kutoka nje ya Bara la Afrika.
10
Waziri Mkuu akizungumza  jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu mara baada ya kufungua  kongamano la Kimataifa la Wakuu wa Taasisi za Takwimu kutoka  nchi 32 za Afrika na 18 za nje ya Bara la Afrika.
11
Waziri Mkuu akizungumza akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Taasisi za Takwimu kutoka  nchi 32 za Afrika na 18 za nje ya Bara la Afrika waliohudhuria Mkutano wa siku 3 wa Takwimu  jijini Dar es salaam.
……………………………………………………..
Habari Picha- na Aron Msigwa/MAELEZO.
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda amesema kuwa Serikali itaendelea  kutoa kipaumbele katika matumizi ya takwimu sahihi na kuweka mifumo mizuri ya kuwarahisishia  wananchi na taasisi mbalimbali kupata takwimu za masuala mbalimbali kutoka Serikalini ili  ili waweze kupanga mpango ya maendeleo.
Akifungua  Kongamano la Kimataifa la Siku 3 la Wakuu wa Taasisi za Takwimu wa nchi 38 za Afrika na 18 kutoka nje ya Bara la Afrika leo jijini Dar es salaam Mhe. Pinda amesema kuwa nchi za Bara la Afrika ili ziweze kuwa na maendeleo endelevu yanayotafsiriwa lazima zitoe kipaumbele katika matumizi ya Takwimu sahihi.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika zilizopiga hatua kubwa katika kuweka mifumo ya kurahisisha upatikanaji wa takwimu za masuala mbalimbali yakiwemo ya Idadi ya watu, takwimu za masuala ya Afya na masuala mbalimbali yanayohusu shughuli mbalimbali za uchumi wa Kaya binafsi.
“ Mpango wowote ambao hautumii takwimu sahihi  hauwezi kuzaa matunda, Lengo letu Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na takwimu sahihi kuhusu idadi ya wananchi wetu, sekta ya afya, Elimu, Biashara, Kilimo na mifugo yetu ili tuweze kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili” Amesisitiza.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa Takwimu sahihi katika Bara la Afrika hususani nchini Tanzania  katika masuala ya Kilimo, Chakula na Mifugo kutasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima na wafugaji  na kuwawezesha  kupunguza idadi ya mifugo waliyonayo kwa  kuwa na ufugaji wenye manufaa na endelevu.
Ametoa wito kwa nchi za Afrika kuendelea kujenga taasisi imara za Takwimu na kuongeza bajeti za kugharamia uwekaji wa mifumo rafiki ya upataji wa takwimu za masuala mbalimbali ili kuwawezesha wananchi  kupata takwimu bila vikwazo na kuweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuijengea uwezo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake.
Aidha, ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoa takwimu rahisi zinazoeleweka na kundi kubwa la watumiaji ametoa na kutoa wito kwa  wadau mbalimbali kutoka sekta ya Umma na Binafsi, viongozi  na wanasiasa kujenga utamaduni wa kutumia takwimu kutoka vyanzo sahihi ili taasisi wanazoziongoza ziwe imara na zenye matokeo.
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu (ISI) Bw. Vijay Nair akizungumza kabla ya uzinduzi wa  Kongamano hilo la Kimataifa amesema kuwa ili kujenga jamii Imara yenye Ubunifu na inayolenga kupata mabadiliko lazima matumizi ya takwimu sahihi yazingatiwe.
Amesema kuwa Taasisi anayoiongoza ya ISI imekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi ya Takwimu sahihi, kujenga taasisi imara zenye wataalam wenye weledi katika masuala ya Takwimu katika nchi mbalimbali za Afrika.
Ameeleza kuwa taasisi yake imekuwa ikifanya kazi ya kuendesha Warsha na Makongamano katika nchi mbalimbali duniani hasa zile zinazungumza lugha ya Kiingereza na Kifaransa kwa kuwakutanisha wakuu wa taasisi na viongozi wengine wakuu wa ngazi ya mawaziri ambao hukutana kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu umuhimu wa matumizi ya takwimu kwa maendeleo ya nchi zao.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua Kongamano hilo la Kimataifa amesema kuwa Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika kuimarisha uwazi katika matumizi ya Takwimu sahihi.
Amesema kuwa licha ya kuwepo kwa tafsiri tofauti ya neon masikini kati ya nchi moja na nyingine,  Ofisi ya Taifa ya Takwimu  inaendelea kuhuisha takwimu mbalimbali ili ziweze kuakisi na kukidhi mahitaji  ya sasa ya matumizi ya wadau mbalimbali kitaifa na Kimataifa.
“Sisi kama Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania tunaendelea kuimarisha shughuli zetu ili kuendelea kujenga uchumi imara kwa takwimu sahihi, tumeendelea kutoa na kubainisha viashiria  vya ukuaji wa uchumi wetu kwa ngazi ya taifa, kutoa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi pamoja na taarifa za Sekta mbalimbali nchini” Amesema.

Comments