Monday, April 27, 2015

CHAMA CHA MAPINDUZI KIMEPOKEA KWA MASIKITIKO MAKUBWA KIFO CHA- BRIGEDIA JENERALI HASHIM MBITA

MbittaChama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa TANU na Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Africa – Liberation Committee of the African National Unity (OAU), Brigedia Generali Hashim Mbita.
Brigedia Generali Mbita alifariki jana Aprili 26, 2015 katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Ndugu Nape Nnauye amemwelezea Marehemu Mbita kama mmoja wa viongozi ambao wameifanyia nchi yetu makubwa na kwa miaka mingi. 
“Kiwango cha utumishi wa Ndugu Hashim Mbita ni cha kutukuka na kwamba mchango wake katika kuijenga TANU na CCM pamoja na ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika utaendelea kuishi mioyoni mwetu daima” amesema Ndugu Nape na kuongeza:
“Misingi ya Chama Chetu CCM na taifa letu tunayojivunia leo ilijengwa kwa jitihada na kwa kujitoa kwa hali ya juu kwa waasisi wetu akiwemo Ndugu Mbita na kwamba faida ya matunda yake yataendelea kuinufaisha CCM na Taifa kwa miaka mingi ijayo”.
Chama Cha Mapinduzi kinaungana na familia ya Ndugu Mbita katika kuomboleza kifo na msiba wa ndugu yetu huyu, nawaomba watambue kuwa msiba wa Ndugu Mbita ni msiba wa CCM, watanzania na Afrika kwa nzima, ambao kwa pamoja tumepoteza busara yake wakati tulipokuwa tunahitaji zaidi.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu, aiweke peponi roho ya Ndugu Hashim Mbita. Amin”.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano na Umma,
Chama Cha Mapinduzi
27 Aprili, 2015

No comments: