MBOWE AENDA ZIARA YA SIKU TANO MIKOANI.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameanza ziara ya siku sita kwenye mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kagera.
Ziara hiyo inalenga mwendelezo wa uzinduzi wa programu ya FTP maalum kwa ajili ya mafunzo ya uzalendo kwa vijana, shughuli ambayo amekuwa akiifanya tangu Januari mwaka huu.
Taarifa kwa vyombo vya habari jana iliyotolewa na Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, ilisema ziara hiyo aliianza jana katika Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.
Alisema ziara hizo zitaambatana na mikutano ya hadhara wilayani Bariadi, Shinyanga kabla ya kwenda wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza.
Maeneo mengine atakayozindua programu hiyo ni Bukoba Mjini kisha Kyerwa na kwamba katika maeneo yote wamelialika Jeshi la Polisi kutoa elimu ya ulinzi shirikishi na polisi jamii.
Makene alisema pia, wameialika Taasisi ya Kupambana na kuzia Rushwa (Takukuru) ili kutoa elimu ya kupambana na kuzuia rushwa hasa wakati wa uchaguzi.
Aidha, alisema viongozi wengine wajuu wa chama hicho wataendelea na programu ya uzinduzi wa mafunzo ya kukiandaa chama kushinda dola na kuiongoza serikali, kwenye mikoa ya Tanga, Shinyanga na Mbeya.
Alifafanua kuwa Makamu Mwenyekiti Taifa Bara, Prof. Abdallah Safari, atakuwa Korogwe Mjini na kuzindua mafunzo hayo kwa viongozi wa Korogwe mjini na vijijini kisha kufanya mkutano wa hadhara Korogwe mjini.
Alisema, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, atazindua mafunzo wilayani Bariadi na pia atakuwa na mkutano wa hadhara Bariadi na Maswa.
Kadhalika, alisema Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, atazindua mafunzo hayo wilayani Mbalizi na kufanya mkutano wa hadhara Njombe mjini.

Comments