Wednesday, April 22, 2015

UCHAGUZI UJAO MABADILIKO MAKUBWA, SURA ZA VIJANA KUTAWALA HASA KATIKA UBUNGE

Mkwawa
Mjumbe wa mkutano  mkuu Taifa  (CCM) kupitia mkoa mpya wa Njombe ,Hassan Mkwawa akizungumza na mwandishi wa habari David John.
…………………………………………………………………………………..
MJUMBE wa mkutano  mkuu Taifa  (CCM) kupitia mkoa mpya wa Njombe ,Hassan Mkwawa amesema kuwa  uchaguzi mkuu wa mwaka huu watanzania watarajie mabadiliko makubwa ya viongozi na hasa wabunge , kwani kutakuwa na sura nyingi za vijana.
Amesema vijana wengi wameonesha nia  na kiu kubwa ya kutaka mabadiliko hivyo kutokana na hali hiyo kutakuwa na changamoto za kutosha kutoka kwa vijana.
Kauli ya mjumbe huyo ameitoa jana jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake kuhusiana na mtazamo wake juu ya uchaguzi wa mwaka huu.
Mkwawa alisema kuwa vijana wana ari kubwa na wanauwezo wa kufanya kazi ,na wapo ambao tayari wapo  Serikalini na  wanachapakazi nzuri,hivyo wananchi watarajie mabadiliko hayo.
“uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na mabadiliko makubwa na vijana wengi watakuwa wabunge na wengi watatokana na Chama cha Mapinduzi CCM”alisema Mkwawa.
Aliongeza kuwa hivi sasa watanzania wanataka mtu mwenye uwezo mkubwa wa kupambanua mambo ambaye anaweza kusimama jukwaani na kuwaeleza wananchi kwa namna atakavyo weza kuwaletea maendeleo na si kumnyoshea mwingine kidole kwa kushindwa kwake.
Alisema kuwa wananchi  wamechoka na siasa za kumwangalia mtu usoni na ndiyo maana katika uchaguzi wa mwaka 2010 sura nyingi za wazee hazikupata nafasi ya kurudi katika nafasi zao za uongozi kwakuwa walishindwa kufanya yale wananchi waliwatuma kufanya
Akizungumzia ujio wa Chama kipya cha ACT –wazalendo  alisema kuwa chama hicho kinaonekana kukusanya watu wengi katika mikutano yake kutokana na wengi wao kutaka kumuona Zitto Kabwe ambapo mara zote walikuwa wakimuona kwenye vyombo vya .
Alisema kuwa katika mikutano hiyo kuna watu ambao wanakwenda kusikiliza kinachozungumzwa kweli na wengine wanakwenda kumuona Zitto Kabwe na kundi lingine linakwenda kutimiza wajibu lakini, kiukweli kutokana na uwezo ambao alikuwa akionesha bungeni ndiyo unafanya uvute watu katika mikutano hiyo.
“Zitto ni kijana na ameonesha uwezo mkubwa wa kiongozi kiasi kwamba alikuwa akiibua hoja nyingi bungeni,hivyo kuna vijana wengi ambao wanauwezo mkubwa wa kuongoza watu,ambapo wengine akina January Makamba ,Said Mtanda, na wengine wengi,alisema Mkwawa
Aidha alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kitashinda kwa kishindo kwani utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi umekuwa wamafanikio kwa kiasi kikubwa na hata wakati wa kampeni utakapo fika makada na viongozi mbalimbali watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuelezea mafanikio hayo mbele ya wananchi.

No comments: