Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana akisisitiza jambo wakati akiongea na watoto pamoja na walezi wa kituo cha Malezi na Makuzi ya Watoto cha Mtambani, Mlandizi wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani.
(Picha zote na Hassan Mabuye)
Baadhi ya watoto wa kituo cha Malezi na Makuzi ya Watoto cha Mtambani wakiwa katika kikao hicho.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana akisisitiza jambo wakati akiongea na wanachuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.
Wanachuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana.
………………………………………………..
Na Hassan Mabuye
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana amefanya ziara ya kutembelea kituo cha kulelea Watoto Wilayani Kibaha mkoa wa Pwani kwa lengo la kuangalia maeneo ambayo yanahitaji maboresho pamoja na kujionea hali halisi ya uendeshaji wa vituo vya kulelea Watoto.
Katika ziara hii Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea kituo cha Malezi na Makuzi ya watoto Kilichopo katika kata ya Mtambani Mlandizi jumatatu tarehe 27 Aprili 2015, ambapo aliongea na Walezi na wasimamizi kukienzi na kukitunza kituo hicho. Aidha Mheshimiwa Pindi Chana amewahusia wasimamizi na wazazi kuyapa kipaumbele mambo yanayohusu Watoto kuanzia kwenye familia na kuyaweka katika bajeti za kila siku za familia kwani taifa la kistaarabu linajengwa kuanzia kwa watoto wadogo.
Mheshimiwa Naibu Waziri alifanikiwa pia kukutana na wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha ambapo aliwahusia vijana kuzingati masomo yao wakati wazazi bado wana nguvu za kuwasomesha. “Unadhani siku hizi ukikimbia shule au kutoroka masomo unamkomoa nani, mzazi au mwalimu? Unajikomoa mwenyewe sababu baadae wewe ndo utabeba majukumu na pengine ndio utakuwa mzazi na maisha ya sasa ni elimu na ujuzi” alisisitiza Mhe. Pindi Chana.
Aidha Mheshimiwa Pindi Chana katika ziara hii alikutana na vikundi vya Wanawake walionufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Wanawake Tanzania eneo la Picha ya Ndege Kibaha.
Comments