Wednesday, March 13, 2013

MANISPAA YA KINONDONI KUKUSANYA BILIONI 156 2013/2014

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akizungumza wakati wa kikao cha Bajeti cha Manispaa hiyo kilichofanyika jana (Machi 12) katika ofisi za Manispaa hiyo, Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu wake, Songoro Mnyonge na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mhandisi Mussa
  Natty.
 002 (2) 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty akizungumza wakati wa Kikao cha Bajeti cha Manispaa hiyo kilichofanyika katika ofisi za Manispaa hiyo, Dar es Salaam jana (Machi 12). Katikati ni Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda na Naibu wake, Songoro Mnyonge.
………………………………………………………………..
MANISPAA ya Wilaya ya  Kinondoni inatarajia kukusanya  zaidi ya sh bilioni 156 kwa ajili ya  matumizi ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo katika manispaa hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Akizungumza  wakati wa kupitisha bajeti Manispa hiyo, jijini Dar es Salaam jana,
Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda alisema kuwa fedha hizo zinatarajiwa kukusanywa katika vyanzo mbalimbali vya mapato katika manispaa hiyo ikiwa ni pamoja na michango ya wananchi na ruzuku kutoka  serikali kuu.
“Wakurugenzi mlipata shida sana wakati wa kupitisha bajeti hii kwa waheshimiwa madiwani lakini hiyo yote ni kwa ajili ya kujenga halmashauri ya manispaa ya Kinondoni wananchi wanahitaji kuona maendeleo na kuwa na bajeti yenye vipaumbele muhimu katika manispaa,”alisema Mwenda.
Mwenda alisema kati ya fedha hizo  sh bilioni 49.2 zinazotarajiwa kutokana na mapato ya ndani huku sh bilioni 1.5  zitakuwa ni michango ya wananchi, ambapo serikali kuu imetoa ruzuku ya sh bilioni  91.1 na  sh bilioni 15 zitatolewa na benki ya CRDB kwa ajili ya upimaji wa viwanja vya Mabwepande.
Alisema  katika sh bilioni 91.1 za ruzuku kutoka serikali kuu, sh bilioni 66.4 ni kwa ajili ya mishahara, sh bilioni 8.3 ni matumizi ya kawaida  na sh bilioni 16.2 ni ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Aliongeza kuwa bajeti ya mwaka 2013/2014 ni mwendelezo wa halmashauri kutekeleza Malengo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Naye diwani wa Sinza Renatus Pamba (Chadema), alisema bajeti hiyo imepita bila kupigwa na wajumbe kutokana na bajeti kuwa shirikisha ambapo fedha nyingi zimetengwa kwa ajili ya kusaidia wananchi  kwa kuziweka katika miradi ya maendeleo.
“Bajeti ya mwaka huu ni ya kihistoria katika manispaa ya Kinondoni  tofauti na tulivyoikuta tumekaa katika kikao kwa kutengwa katika kamati mbalimbali kuijadili kwa muda wa siku tano,fedha zilizokwenda kwenye miradi ya maendeleo ni nyingi ambazo zitasaidia kuendeleza manispaa,”alisema Pamba.

No comments: