Friday, March 01, 2013

Mkurugenzi Mkuu NHC achaguliwa Bodi ya Mikopo ya Nyumba Afrika


MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Nehemia Kyando Mchechu, amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Mikopo ya Nyumba ya Umoja wa Afrika (AUHF) kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi huu. Atatumikia katika Bodi hiyo hadi Oktoba, 2014.
Uchaguzi wa Mchechu na Wajumbe wenzake nane wa Bodi ya AUHF kushika nafasi hiyo muhimu barani Afrika, umefanyika hivi karibuni.
AUHF hivi sasa ina wanachama  38 kutoka nchi 17 duniani, za Botswana, Ghana, Kenya, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Gambia, Uganda, Uingereza, Marekani na Zimbabwe.
 AUHF ilianzishwa kama ya wanachama wakopeshaji wa mikopo ya nyumba mwaka 1984. Hivi sasa ina wanachama 38 kutoka mataifa 17, ikiwa na lengo la kuboresha ustawi wa mikopo ya nyumba barani Afrika kwa kujenga uwezo wa kitaasisi kwa taasisi husika na kufanya kazi na serikali za nchi wanachama kuwa na sera za maendeleo zenye mazingira bora ya soko.
Kupitia mikutano yake na kazi inazofanya sambamba na tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa mbalimbali inazozitoa kwa wanachama, AUHF imekuwa kiongozi mkuu katika kustawisha masoko ya mikopo ya nyumba kwaajili ya jamii ya kiafrika.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuingia katika bodi ya Shirika hilo, Mchechu alisema kuwa maendeleo ya soko la mikopo ya nyumba nchini Tanzania yatakuwa kwa kasi zaidi sasa.
“Tunaamini ya kwamba, ujuzi tulio nao hapa Tanzania unaweza kuwa na mchango mkubwa saana katika maendeleo ya sekta ya nyumba barani Afrika na Duniani. Faida ya kuwa na jumuiya kama hii ya kikanda ni kwamba tunaweza sasa tukabadilishana uzoefu na ujuzi kutoka maeneo yote,”alisema Mchechu.
Mchechu amechaguliwa kuingia katika Bodi hiyo ya Afrika, sambamba na Mtanzania mwingine Oscar Mgaya, ambaye ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba (TMRC).
TMRC ni kampuni binafsi ambayo ilianzishwa kwa mkopo wa dola milioni 30 kutoka Benki ya Dunia, ili kufanikisha upatikanaji wa mtaji wa mikopo ya nyumba hapa nchini.
Benki ambazo mpaka sasa zimenunua hisa katika kampuni hiyo kuwa ni CRB, Azania Bank, TIB, Exim Bank, Dar es Salaam Community Bank, NIC Bank, Banc ABC, NBC, People Bank of Zanzibar na BoA.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam Mgaya alisema kuwa “AUHF ina historia ndefu ya kuchagiza maendeleo ya mifumo ya mikopo barani Afrika. Mwenyekiti wa Bodi hiyo ni Colin Chimutsa, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya  Biashara ya Zimbawe (CBZ), ametumikia pia nafasi ya ujumbe chini ya Mwenyekiti Mstaafu, Reginald Motswaiso.
Makamu Mwenyekiti ni Charles Bonsu, ambaye ni Meneja Mkuu wa mikopo na masuala ya wateja wakubwa wa Benki ya Biashara yenye mtandao mkubwa ya HFC ya Ghana.
Mweka Hazina ni Cas Coovadia, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Kibenki ya Afrika Kusini, pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya utoaji mikopo ya nyumba, amechaguliwa tena katika bodi hiyo kwani alikuwapo katika bodi iliyopita.
 Katibu Mkuu, Oscar Mgaya, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba (TMRC, yeye ni mpya katika bodi hiii.
Reginald Motswaiso, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa la Botwana, amechaguliwa tena kuingia katika bodi hii mpya baada ya kutumikia kama Mwenyekiti katika Bodi iliyopita.
Mwingine ni Manilall Seetohul, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Nyumba ya Mauritius naye kama walivyo wengine amechaguliwa tena kuingia katika bodi hii, baada ya kutumikia katika bodi iliyopita..
Katika orodha hiyo ya wajumbe wa bodi pia yupo Madu Hamman, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Fedha na Utawala wa Kampuni ya Abbey Building Society PLC ya nchini Nigeria.

No comments: