Friday, March 01, 2013

FBI wawasili Zanzibar kufanya uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa kumpiga risasi, Padri Mushi

 Waziri wa mambo ya Ndani,Dk Emmanuel Nchimbi
 Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa
--- 
ASKARI wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), wamewasili Zanzibar kufanya uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa kumpiga risasi, Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki.
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kwa simu jana kuwa wapelelezi wa kigeni wamewasili Zanzibar na tayari na wameanza kazi hiyo.Wapelelezi hao wameingia kazini kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwasaka wauaji wa padri huyo aliyepigwa risasi Februari 17, mwaka huu.
Padri Mushi aliuawa asubuhi alipokuwa akienda kuongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu Teresia, Beit el Raas, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuzikwa Kitope, Kaskazini Unguja Februari 20, mwaka huu.
“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” Kamishna Mussa alisema bila ya kutaja wanatoka nchi gani.
Pia Kamishna Mussa hakutaka kueleza ni lini wapelelezi hao walifika Zanzibar na idadi yao kwa maelezo kwamba hizo ni siri za Polisi na zikivuja, zitaingilia uchunguzi wanaoufanya.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya Serikali, vililithibitishia gazeti hili kuwa FBI walikuwa wameanza kuwasaka wauaji wa Padri Mushi.
Kutua kwa wapelelezi hao wa Marekani kunafuatia kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za rambirambi baada ya mauaji ya Padri Mushi kuwa ameliagiza Jeshi la Polisi kutumia nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya usalama vya ndani na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.Kwa Habari zaidi Bofya na Endelea......>>>>>>>>

No comments: