HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, 28 FEBRUARI, 2013
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi
wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuwasiliana kupitia
utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea wa kufanya hivyo kila mwisho wa
mwezi. Leo nimepanga kuzungumza nanyi mambo matatu; yaani Mpango wa
Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,
Uhusiano wa Waislamu na Wakristo na Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha
Nne.
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Ndugu Wananchi;
Tarehe 8 Februari, 2013 kule Addis
Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban
Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Nkosozana
Dlamini Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini
kutia saini Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake. Pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo zilikuwepo nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Sudani Kusini,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Angola, Zambia na Tanzania
ambazo ni jirani ya Kongo. Nchi za Ethiopia, Msumbiji na Afrika ya
Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zilitia saini kama
wadhamini. Ethiopia kwa nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Umoja
wa Afrika na Msumbiji kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC). Nchi wanachama wa Mkutano wa Ukanda wa Maziwa
Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo ni Mwenyekiti wake wa sasa.
Afrika ya Kusini ilishirikishwa kwa kuwa taifa kubwa na linalotegemewa
katika ukanda wetu.
Mpango huu ni jitihada nyingine ya
kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ipate amani ya kudumu. Kama
tujuavyo, tangu mwaka 1997 wakati wa vita vilivyosababisha kuondolewa
kwa Rais Mobutu Seseseko mpaka sasa nchi hiyo rafiki na jirani haijapata
amani na utulivu wa kudumu. Kumekuwepo jitihada na mipango kadhaa ya
kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya muda fulani machafuko hutokea
tena na mipango hiyo kuvurugika. Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni
5.4 wamepoteza maisha na watu wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi
yao. Pia kumekuwepo na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto
pamoja na mali nyingi kuharibiwa au kuporwa.
Ndugu Wananchi;
Comments