Wednesday, March 27, 2013

HUYU NDIYE DEREVA ALIYEMGONGA TRAFIKI ENEO LA BAMAGA

   

ANAYEDAIWA kumuua askari wa kikosi cha usalama barabarani wiki iliyopita, Elikiza Nnko, Jackson Stephen Fimbo, jana alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na makosa ya matatu, likiwemo kosa la kuingilia msafara wa Rais. 
Mbele ya Hakimu Mkazi Kwey Lusema, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Lasdilaus Komanya, alilitaja kosa la kwanza kuwa ni la kusababisha kifo cha trafiki huyo kwa kumgonga na gari alilokuwa alikiliendesha.
Ilidaiwa kuwa Machi 18, mwaka huu, katika Barabara ya Bagamoyo kwenye taa za Bamaga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili T328 BML aina ya Land Lover Discovery, alitenda kosa hilo.
Komanya alidai mshtakiwa huyo aliendesha gari hilo kwa mwendo wa hatari katika barabara hiyo jambo ambalo huhatarisha usalama wa raia, hivyo kumgonga askari huyo aliyezikwa Alhamisi iliyopita.
Alidai kosa la pili ni kuingilia msafara wa kiongozi, kuwa tarehe iliyotajwa hapo juu, mshtakiwa hakutii maelekezo yaliyokuwa yakitolewa kwa ishara na askari huyo (marehemu Elikiza) ambaye alikuwa na wajibu wa kuyasimamisha magari kwa njia ya ishara.
Komanya alidai shtaka la tatu ni la kushindwa kutoa taarifa za kusababisha ajali katika barabara hiyo.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikanusha mashtaka hayo na Komanya alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, anaomba tarehe ya kuja kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa.
Kwa upande wake hakimu Rusema alisema ili apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya sh milioni 2 hata hivyo mshtakiwa alitimiza masharti hayo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 15 itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima na wenzake, kwa sababu Kibanda bado amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, hivyo kuahirishwa hadi Aprili 29 mwaka huu.

No comments: