Wednesday, March 20, 2013

LWAKATARE ATUPWA GEREZANI HADI APRIL 3 BAADA YA KUFUNGULIWA MASHITAKA UPYA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewafutia kesi ya makosa ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka( DPP), Dk Eliezer Feleshi kuwasilisha hati ya kuwafutia kesi hiyo washitakiwa kwa sababu hana haja ya kuendelea nayo. 
Sambamba na hilo, DPP ilimfungulia kesi ya makosa ya ugaidi upya Lwakatare na Ludovick ambapo kesi hiyo mpya namba Na.6/2013 ambapo imepangiwa kwa hakimu mpya Aloyce Katemana. 
Katika kesi ya ugaidi Na.37/2013 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Lwakatare na wenzake Machi 18 mwaka huu, ambayo ilifutwa saa tatu asubuhi na ambayo ilikuwa imekuja kwa ajili ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru kuitolea uamuzi wa ama wa kuwapatia dhamana washitakiwa au la, hakimu Mchauru alijikuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwa sababu mawakili viongozi wa serikali Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo waliwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambapo kifungu hicho kina mpa mamlaka DPP, kuifuta kesi yoyote ya jinai muda wowote kabla ya haijatolewa hukumu na uamuzi huo wa DPP haujahojiwa na mtu yoyote. 
 “Kwa kuwa kesi hii Na.37/2013 ilifunguliwa na upande wa jamhuri MAchi 18 mwaka huu, na leo kesi hii ilikuja kwa ajili ya mahakama kutolea uamuzi wa maombi ya washitakiwa kupatiwa dhamana au la pamoja na maombi mengine…mahakama hii inasema haitaweza kutoa uamuzi wake kwa sababu DPP amewasilisha hati ya kutotaka kuendelea kuwashitaki washitakiwa na hivyo mahakama hii inawafutia kesi washitakiwa wote”alisema hakimu Mchauru. 
Baada ya hakimu Mchauru kuwafutia kesi, askari kanzu waliwakamata tena washitakiwa hao na kuwaweka chini ya ulinzi wa gari la polisi na ilipofika saa 4:20 asubuhi, washitakiwa hao wakiwa chini ya ulinzi mkali wa wana usalama waliingizwa tena katika ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo mbele ya hakimu mkazi mwingine Aloyce Katemana. 
Mawakili Wakuu wa Serikal, Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Wakili Mwanadamizi wa Serikali Peter Mahugo walidai kuwa kesi hiyo nimpya na imepewa Na.6 ya maka huu, ambapo washitakiwa ni Lwakatare na Ludovick wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Profesa Abdallah Safari na Peter Kibatara na kwamba hati hiyo mashitaka ina jumla ya mashitaka manne ambapo shitaka la kwanza linaangukia kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na makosa matatu yote yanaangukia kwenye Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002. Wakili Rweyongeza alililata kosa la kwanza ambalo linawakabili washitakiwa wote kuwa ni la kula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru Denis Msaki ambaye ni Mhariri wa habari wa Gazeti la Mwananchi ambalo ni kinyume na kifungu cha 227 cha sheria hiyo. SOURCE: MPEKUZI HURU wa  http://www.mpekuzihuru.com/2013/03/ripotilwakatare-atupwa-gerezani-hadi.html

No comments: