Tuesday, August 18, 2015

NHIF YAINGIA MKATABA NA JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA JWTZ

unnamed (1)
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Michael Mhando na Mkuu wa Huduma za Matibabu Jeshini Brigedia Denis Raphale Janga wakitia saini mkataba wa ushirikiano ambapo Mfuko utatumia vituo vya matibabu vya Jeshi kutibu wanachama wake.
unnamed
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Michael Mhando na Mkuu wa Huduma za Matibabu Jeshini Brigedia Denis Raphale Janga wakikabidhiana mkataba.
………………………………………………………….
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeingia mkataba na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambapo wanachama wa mfuko huo na wategemezi wao watapata huduma za matibabu katika hospitali za jeshi nchini kote.
Mkataba huo wa miaka mitatu uliosainiwa jana unalenga kupanua wigo wa vituo vya matibabu na kuanzisha ushirikiano wa kihistoria baina ya pande mbili hizo.
Akizungumza wakati wa kutia saini mkataba huo Mkuu wa Huduma za Afya Jeshini Brigedia Denis Raphael Janga, amesema amepokea kwa furaha mkataba huo kwa kuwa utawapa nafasi ya kutoa huduma bora kwa kundi kubwa la wanachama wa NHIF ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma katika vituo vya jeshi vilivyo karibu nao.
Ameahidi kushirikiana kwa karibu na uongozi wa NHIF ili kuhakikisha wanachama na wategemezi wao wanapata vipimo na dawa wakati wote watakapokwenda kwenye vituo hivyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Michael Mhando amesema NHIF kwa muda mrefu fursa ya kufanya kazi na JWTZ katika sekta ya matibabu na kwamba mkataba huo unafungua historia mpya ya ushirikiano baina ya taaisi hizo wa kujenga nchi kwa pamoja.
Amesema ili kuhakikisha kuwa mkataba huo unakuwa na manufaa kwa pande zote mbili Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya utaandaa mafunzo maalumu kwa watoa huduma wa vituo vya jeshi ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya kuhudumia wanachana wa NHIF watakaokwenda kupata huduma katika vituo hivyo.
Mhando ameongeza kuwa NHIF itaendelea kushirikiana na uongozi wa JWTZ ili kukamilisha taratibu za kiutawala zitakazowawezesha wanaejeshi na familia zao kujiunga na kunufaika na matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Aidha ameushauri uongozi wa JWTZ kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba, ukarabati na dawa na vitendanishi inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kuhakikisha kuwa vituo vya matibabu vinavyomilikiwa na JWZT vinakuwa na mazingira mazuri na vitendea kazi vinavyotakiwa.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lina vituo vya matibabu vya ngazi mbalimbali zaidi ya kumi na nane nchini kote.
Post a Comment