Tuesday, December 16, 2014

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA WAFANIKIWA KWA ASILIMIA 98.

unnamed
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Hawa Ghasia akiwaeleza waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam kuhusu mafanikio ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana kote nchini ambapo umefanikiwa kwa asilimia 98%,kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Jumanne Sagini.
unnamed2
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Hawa Ghasia akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam uliolenga kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa Serikali uliofanyika jana kote nchini.
………………………………………………………………………………….
Frank Mvungi- maelezo
Serikali imesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana Kote Nchini umefanikiwa kwa Zaidi ya asilimia 98% katika Mikoa yote .
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia wakati wa mkutano na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam uliolenga kutoa ufafanuzi kuhuzi mafanikio ya uchaguzi huo.
Akifafanua Mh. Ghasia amesema kwa kiwango kikubwa wananchi walijitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wao katika ngazi ya Mitaa,Vijiji, na Vitongoji.
Akizungumzia mafanikio ya Uchaguzi huo Mh. Ghasia alitaja Mikoa ambayo uchaguzi umefanyika katika Halmashauri na Kata zote kuwa ni Arusha,Mbeya,Kagera,Njombe,Singida,Lindi,Ruvuma,Katavi na Geita.
Mikoa Mingine iliyofanya vizuri katika uchaguzi huo ni Iringa,Dodoma,Mtawara ambapo Mh. Ghasia aliwapongeza Viongozi na wataendaji wote wa Mikoa na Halmashauri hizo pamoja na wananchi kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya hadi kufanikisha uchaguzi huo.
Akitoa ufafanuzi Zaidi kuhusu maboresho yaliyofanywa na Serikali katika uchaguzi huo Mh. Ghasia amesema kuwa mojawapo ni kuwepo kwa utaratibu wa kupiga kura kwa kutumia karatasi maalum zilizochapishwa kitu ambacho katika uchaguzi uliopita hakikuwepo.
Akizungumzia Mikoa ambayo baadhi ya Halmashauri zimeahirisha uchaguzi ama Halmashauri yote au sehemu ya Kata zake kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kufika kwa vifaa vya kupigia kura Mh.Ghasia aliitaja kuwa ni Kilimanjaro katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Hai,Manyara katika Halmashauri za Hanang na mbulu.
Mikoa Mingine ni Morogoro katika Halmashuri ya Wilaya ya Ulanga na Mvomero,Mkoa wa Shinyanga Halmashauri ya Wilaya ya Msalala,Mkoa wa Simiyu Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Itilima ambapo Mikoa mingine ambayo kasoro ndogondogo zilijitokeza na kupelekea uchaguzi kuahirishwa katika baadhi ya Kata ni Kigoma,Mwanza,Tabora,Tanga,Mara,Rukwa,Pwani na Dar es salaam.
Akizungumzia Hatua zitakazochukuliwa na Serikali kufuatia dosari zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo Mh. Ghasia amesema Mikoa yote imetakiwa awasilishe taarifa rasmi na kamilifu kuhusu yaliyojitokeza katika Halmashauri zao ambapo Wizara yake itachambua taarifa hizo ili kubaini chanzo cha kasoro zilizojitokeza ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kuhusu Halmashuri ambazo hazikufanya uchaguzi kutokana na kasoro mbalimbali Mh. Ghasia amesema kwa mujibu wa Kanuni zinatakiwa kurudia uchaguzi huo ndani ya siku saba kama kanuni za uchaguzi huo zinavyoelekeza.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Jumanne Sagini alitoa wito kwa vyombo vya habari kuweka uzalendo mbele katika kuripoti habari za uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kusaidia Taifa kukamilisha mchakato huo muhimu.
Akifafanua Sagini amesema ni vyema vyombo vya Habari vikaonyesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uchaguzi huo pamoja na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya Mitaa,Vijiji, na Vitongoji ulifanyika tarehe 14/12/2014 kote nchini ambapo taarifa za awali zimeonyesha kuwa zoezi la kupiga kura lilienda vizuri katika Mikoa Mingi.

No comments: