BENKI ya Posta Tanzania (TPB) Tawi la Mbeya, imetoa semina kwa Wajasiriamali wa mkoa ikiwa na lengo la kuwaongezea ujuzi kwenye biashara zao. Semina hiyo ya siku moja imefanyika kwenye ukumbi wa Mtenda Sunset mjini Mbeya na kufunguliwa na Mkuu wa Wilaya, Profesa Norman Sigallah.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa semina hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi, Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa wajisiriamali kutoogopa kukopa kwenye mabenki ili kukuza mitaji yao na hatimae biashara zao.
Prof. Sigallah alitoa changamoto kwa wajasiriamali kuhakikisha biashara zao zinaubora unaotakiwa ili kuweza kujenga imani na ushindani kwenye soko. Mkuu huyo wa Wilaya alitoa changamoto kwa benki ya Posta kuweka dawati maalum la wataalam watakaotoa ushauri kwa wajasiriamali pindi wanapokuja kuomba mikopo. Aliwashauri wajasiriamali kujiepusha na makundi yenye muelekeo wa kuleta vurugu na kuvunja amani, kwani ili kukua biashara yoyote inahitaji amani na utulivi.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi, akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wajasiriamali hao zaidi ya 150 waliohudhuria semina hiyo, alisema benki yake itaendelea kuboresha huduma zake hasa upande wa mikopo, na pia kuangalia suala la riba zinazotozwa kwa aina tofauti ya biashara.
“Benki yangu itaendelea kuangalia ni namna gani tunaweza kuweka wataalam watakaotoa ushauri mzuri kwa wajasiriamali ili kupunguza mlolongo mrefu wa nenda rudi kwa mkopaji. Hii ni katika jitihada za kuhakikisha kuwa mkopaji anapata mkopo kwa wakati ili kuwahi fursa iliyojitokeza,”.
Akiongea kwa niaba ya wajasiriamali hao, Bi. Joyce Mkongo, aliishukuru sana benki ya Posta kwa kutoa mafunzo hayo kwao,ambayo yamewafungua macho na kuwaondolewa woga wa kutumia huduma za kibenki. Alisema wajasiriamali wengi wanasita kuchukua mikopo kwa hofu kuwa mali zao zitataifishwa pindi watakaposhindwa kulipa mkopo.
Comments