Wageni mbalimbali wanaoshiriki mkutano mkubwa wa kimataifa wa hifadhi ya jamii ulioandaliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha ulioanza leo katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha (AICC) wakifanya usajili kabla ya kuanza kwa mkutano huo. (Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog).
Na Mwandishi wetu
MAKAMU wa pili wa rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, amesema mpango wa serikali ya Tanzania wa hifadhi ya jamii ndio msingi wa sera ya kuondoa umaskini miongoni mwa watu wake ili kulifanya taifa kuwa la kipato cha kati ifikapo 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo wakati akifungua mkutano mkubwa wa kimataifa wa hifadhi ya jamii ulioandaliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na wadau wengine kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya nini cha kufanya kusaidia makundi maalumu katika jamii.
Katika Mkutano huo wa siku tatu unafanyika Katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha (AICC) serikali imefanya maandalizi kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama UNICEF, ILO, UNAIDS na taasisi ya utafiti wa sera za kiuchumi yenye makao makuu nchini Afrika Kusini (EPRI).
Imeelezwa kuwa mkutamo huo umelenga kuchota maarifa mema kutoka Afrika Kusini ya namna ya kutengeneza sera za kuhudumia makundi maalumu ya wanawake, watoto, wazee, wasiojiweza na vijana ili kuboresha maisha yao, ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa serikali wa kuinua kiwango cha maisha miongoni mwa wananchi wake.
Mkurugenzi msaidizi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani na Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Aeneas C. Chuma (kulia) akiwasili kushiriki mkutano huo akiwa ameambatana na Afisa Habari wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Tanzania, Bw. Magnus Minja (kulia) pamoja na Luis Frota kutoka ILO Afrika Kusini.
Balozi Seif Ali Iddi, alisema kwa kuzingatia nia ya serikali ya kuwa taifa lenye kipato cha kati mwaka 2025 serikali inaona haja ya kuangalia sera ili iweze kutoa haki kwa makundi yote kuelekea ustawi wa jamii ifikapo mwaka huo..
“Serikali imechukua hifadhi ya jamii kama mkakati wa kufikia dira ya ukuaji na maendeleo nchini. Kongamano hili limekusudia kuhakikisha kwamba muono unatengeneza hatua stahiki zinazotekelezeka kitaifa kukabiliana na changamoto za umaskini hivyo kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa endelevu na wenye maana kwa wananchi” alisema.
Alisema ili kufikia lengo hilo la uchumi endelevu, serikali inataka kuhakikisha wananchi wake wakiwemo wale maskini na wasiojiweza wanawezeshwa ili kutambua haki zao na kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye nguvu na linalotoa haki sawa kwa wote.
Aidha kuwa taifa linaloangalia mahitaji ya watoto wake kama lishe, afya na elimu ili kuwasaidia kukua kwa furaha, kuwa wazalishaji na kukwepa mtego wa umaskini unazinga kizazi kwa kizazi.
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania Hoyce Temu (kulia) akimwongoza Mkurugenzi msaidizi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani na Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Aeneas C. Chuma kuelekea kwenye chumba maalum cha wageni mashuhuri kabla ya kuanza kwa mkutano. Katikati ni Afisa Habari wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Tanzania, Bw. Magnus Minja.
Balozi Iddi alisema kwamba amefurahi kuona kwamba ajenda za mkutano pia zimegusia kuzungumzia uimarishaji wa utendaji wa pamoja kati ya mipango ya hifadhi ya jamii kama TASAF, Mfuko wa afya ya jamii (CHF) na huduma za jamii zinazotolewa na wizara husika kama wizara ya elimu, afya, maji nakadhalika.
Hata hivyo aliwataka washiriki kuangalia ukusanyaji wa takwimu kuhusu masuala ya hifadhji ya jamii kwani kwa hali ilivyo sasa ukusanyaji huo si mzuri na unazuia maendeleo na uimarishaji wa huduma za jamii.
Alisema ipo haja ya kuboresha mazingira ya utawala ili kuwezesha kuimarisha hifadhi kwa wale waliokwishaipata, kubadili sheria ili kuwaingiza na wale ambao hawajapata huduma za hifadhi ya jamii.
Aliwataka washiriki kuangalia kwa makini changamoto zinazoikumba Afrika na Tanzania katika masuala ya hifadhi na kutolea majibu.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi msaidizi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani (ILO) na Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Aeneas C. Chuma.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni umaskini uliotapakaa ambao unasababisha watu kushindwa kupeleka michango katika hifadhi, misingi ya ukataji kodi ambayo huleta mushkeri kwa fedha za hifadhi, kuwepo kwa kundi kubwa lisilo katika sekta rasmi ya ajira na hivyo kupunguza idadi ya wachangaji katika prgramu zinazohitaji michango mfululizo na mabadiliko ya tabia nchi yanayotishia kuyumba kwa kilimo na ufugaji ambao ndio msingi wa mapato kwa wananchi wengi.
Alisema pia mabadiliko ya tabia nchi yanasababisha milipuko ya magonjwa mbalimbali kama Malaria na magonjwa mengine mapya kama Ebola na Dengue.
Changamoto nyingine ni kuwepo na gharama kubwa za utawala hasa katika siku za mwanzo za uanzishwaji wa mifuko ya hifadhi.
Mkutano huo wenye washiriki zaidi ya 150 una watu wa kariba mbalimbali wakiwemo watengeneza sera, watafiti na waendeshaji wa mifuko ya hifadhi kutoka mataifa ya Kenya, Uganda, Bangladesh, Mozambique, Lesotho, Malawi, Afrika Kusini, Ghana, Ethiopia, Zambia, Sudan Kusini na wenyeji Tanzania.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi msaidizi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani na Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Aeneas C. Chuma kabla ya kuwasili kwa mgeni rasmi Balozi Seif Ali Iddi.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa mwelekeo wa namna ambavyo Tanzania inaweza kuanzisha mfumo wa hifadhi kwa ajili ya watu maskini na wale wenye mahitaji maalumu ili kuwawezesha kupata huduma za afya, elimu na kipato.
Naye Mkurugenzi msaidizi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani na Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Aeneas C. Chuma, amesema Umoja wa Mataifa umefurahishwa na kuwapo kwa kongamano hilo kwani suala la hifadhi ni msingi wa maendeleo katika uchumi wowote endelevu.
Alisema kuwapo kwa Hifadhi ya jamii inayoeleweka na yenye msingi imara husaidia wananchi kukabiliana na mabadiliko yoyote yale ya kiuchumi katika taifa lao.
Alisema shirika hilo katika miaka yote 95 ya uwapo wake inapigania hifadi ya jamii kama njia salama ambayo inahakikisha ukuaji wa jamii unaozingatia uwapo wa jamii inayozingatia ukuaji wa uchumi wenye haki kwa kila mmoja.
Waziri wa Fedha, Mh. Saada Mkuya Salum (kushoto) akiwasili kwenye viwanja vya AICC jijini Arusha kushiriki mkutano mkubwa wa kimataifa wa hifadhi ya jamii ulioandaliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha huku akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dr. Servacius Likwelile (katikati) pamoja na Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Jama Gulaid.
Pamoja na mafanikio ya dunia katika masuala ya afya na elimu, Mwakilishi huyo ameelezea changamoto kubwa inayokabili Tanzania ambayo ni vijana wengi kuingia katika soko la ajira ambalo ni finyu.
Mwakilishi huyo amesema kwamba kuanzia mwaka ujao hadi 2030 nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la sahara wanatakiwa kutengeneza nafasi milioni 5 za kazi kila mwaka ili kuendana na ukuaji wa soko la wasaka ajira.
Alisema kutokana na ukweli huo hatua ya sasa ya Tanzania kutaka kuwa na msingi imara ya hifadhi ya jamii ni muhimu sana ili kukabiliana na mabadiliko yanayokuja katika afya, elimu na ajira.
Wakati huo huo Mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mkurugenzi mkazi wa UNDP Alvaro Rodriguez amesema hifadhi ya jamii ni kitu muhimu kinachofanya watengeneza sera kukaa pamoja kuona namna nzuri ya kufanikisha masuala hayo.
Waziri wa Fedha, Mh. Saada Mkuya Salum (katikati) akiwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) pamoja na Naibu waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Dkt. Pindi Chana wakielekea kumpokea mgeni rasmi Makamu wa pili wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi.
Alisema matukio mbalimbali yanayoharibu ustawi wa jamii kama kuporomoka kwa uchumi duniani, mabadiliko kwenye tabianchi kumefanya kuwepo na haja ya kuhakikisha kwamba kuna misingi imara ya kutoa hifadhi kwa wananchi na kuboresha maisha yao.
Akizungumza katika mkutano huo kabla ya Makamu wa rais kuhutubia, Alvaro alisema kuna changamoto kubwa zinazokabili dunia.
Alipongeza serikali ya Tanzania kwa kuona haja ya kushirikiana na wadau wengine kuona namna bora ya kukabiliana na changamoto za maendeleo katika lengo la kuhakikisha kunauwezeshaji wenye lengo la kuwezesha ustawi wa jamii.
Alisema mada zitakazojadiliwa zitawezesha mwishoni mwa mkutano kuwapo na maazimio yenye kuwezesha kutengenezwa kwa mising bora ya hifadhi ya jamii ili kuwezesha maono ya maendeleo kufikiwa.
Mratibu huyo pia alielezea kuridhishwa kwake na mafanikio yanayopatikana nchini Tanzania kupitia TASAF ya kukabiliana na umaskini uliokithiri na kutoa nafasi ya maskini kuwa na uwezo wa kusonga mbele katika maendeleo ili kufikia maono ya taifa ya maendeleo endelevu yanayojali watu wote 2025 wakati taifa litakapokuwa la kipato cha kati.
Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mkutano mkubwa wa kimataifa wa hifadhi ya jamii ulioandaliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, Makamu wa pili wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dr. Servacius Likwelile mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya AICC jijini Arusha leo.
Makamu wa pili wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi , akisalimiana na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez alipowasili kwenye ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa hifadhi ya jamii.
Mgeni rasmi Makamu wa pili wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi akisalimiana na Mwakilishi wa Shirika la watoto duniani (UNICEF), Jama Gulaid.
Mgeni rasmi Makamu wa pili wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi (katikati) akiwa na Waziri wa Fedha, Mh. Saada Mkuya Salum pamoja na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda wakielekea kwenye ukumbi wa mikutano.
Picha juu na chini ni mgeni rasmi Makamu wa pili wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi, akifungua mkutano mkubwa wa kimataifa wa hifadhi ya jamii ulioandaliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na wadau wengine kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya nini cha kufanya kusaidia makundi maalumu katika jamii ulioanza leo jijini Arusha.
Kwa picha zaidi ingia humu
Comments