UVCCM WAMPONGEZA MHE RAIS JAKAYA KIKWETE KWA HOTUBA YENYE UFAFANUZI WA KUJITOSHELEZA KUHUSU ESCROW

index

Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) inampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa Jakaya Mrisho Kikwete kwa hotuba yake nzuri iliyojaa ufafanuzi bayana wa masuala makubwa ya kitaifa, likiwemo suala la Akaunti ya Escrow ya Tegeta, yaliyoleta mkanganyiko kwa wananchi, aliyoitoa jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee alipozungumza na wazee wa jiji la Dar es salaam.
Sisi Vijana tunampongeza kwa kubariki na kuridhia hatua iliyochukuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Hawa Ghasia za kuwachukulia hatua sitahiki wakurugenzi wazembe waliovuruga Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.
Tunahimiza utaratibu huo uwe endelevu kwa kuendelea kuwachukulia hatua kali wakurugenzi ambao wanapata hati chafu za Ukaguzi pamoja na wale ambao wanashindwa kutimiza wajibu wa kisheria wa kutenga asilimia tano (5) za mapato ya Halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya Vijana.
Pia, Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, (Mb) Mheshimiwa Anna Kajumulo Tibaijuka.
Tunamwomba Mheshimiwa Rais kumteua Waziri mwingine ambaye atamudu wizara hiyo ipasavyo kwa kutatua na kumaliza kabisa migogoro ya ardhi ambayo imeendelea kusababisha vurugu, machafuko na maafa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kama vile Mvomero, Maswa, Kiteto. Tunapendekeza apatikane Waziri ambae muda wake mwingi atakuwa katika maeneo hayo akitafuta suluhu ya kudumu kati ya wafugaji na wakulima, baina ya wafugaji, wakulima na hifadhi, na baina ya wananchi, hifadhi na wawekezaji.
Pia, tunavitaka vyombo vinavyoendelea na uchunguzi, kumaliza na kukabidhi matokeo ya uchunguzi wao katika mamlaka husika mapema ili kutoa fursa kwa maamuzi kufanyika kwa wakati.
Tunavitaka vyombo hivyo kufanya kazi zake kwa weledi na uaminifu mkubwa ili jambo hili lipate maamuzi sahihi lakini pia asionewe mtu na haki itendeke.
Na mwisho tungependa kuwakumbusha wananchi na viongozi kuheshima mgawanyo wa madaraka, na kuheshimu nguvu na mamlaka za kila mhimili wa Taifa, tunaiomba Mamlaka ya Bunge iendelee na utaratibu wake katika kuwashughulikia wale walio kwenye mamlaka zake ambao wamehusika katika kadhia hii ya ESCROW na pia kuitaka mahakama na tume zake kuchukua hatua kulingana na taratibu na miongozo yao.
Tunawaomba Wananchi kuwa makini na kutoruhusu mijadala inayohusu suala hili kutawaliwa na maslahi binafsi ya wafanyabiashara na wanasiasa, ambao wameendelea kushawishi na kushinikiza maamuzi yanayolinda maslahi yao.

Comments