Tuesday, December 23, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA MAKAO MAKUU YA JESHI LA POLISI

imagesTunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu za Krismas na mwaka mpya, wananchi wenye imani ya Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe ambapo uzoefu unaonyesha baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu hasa wa kujipatia vipato na mali.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kipindi hiki cha sikukuu na pale ambapo vitajitokeza vitadhibitiwa kwa haraka. Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu. Hata hivyo, watu wote watakaoenda maeneo ya beach wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka kuzama kwenye maji.
Aidha, tunawakumbusha wananchi kuwa makini katika suala zima la usalama wa maisha na mali zao, hususani kuchukua hatua stahiki na za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao na sehemu mbalimbali za biashara, na watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na pale inapobidi watoe taarifa kwa majirani zao. Wazazi wanakumbushwa kuwa makini na watoto kwa kutokuwaacha watembee peke yao, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao ikiwemo kupotea. Aidha, wazazi waepuke kuwapeleka watoto kwenye kumbi za disko toto ambazo siyo salama.
Vilevile, wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie usalama katika kumbi zao, hawarusiwi kujaza watu kupita kiasi kwenye kumbi hizo, hususani kumbi za disko toto. Aidha, wamiliki wa kumbi za starehe na maeneo mengine yenye mikusanyiko mikubwa ya watu wanakumbushwa kufunga vifaa maalum vya kufuatilia mienendo ya watu wanoingia na kutoka katika maeneo hayo (CCTV kamera).
Pia, Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.
Mwisho, tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za mipango yoyote ya uhalifu watakayoiona ikiendelea mahali popote kwa kuwafichua wahalifu hao ili hatua za kuzuia uhalifu huo ziweze kuchukuliwa mapema. Taarifa zinaweza kutolewa kupitia namba ya simu 0754 78 55 57 au Simu za Makamanda wa Polisi wa mikoa au katika kituo chochote cha Polisi.

No comments: