Tuesday, December 23, 2014

MAKAMPUNI SABA YAJISAJILI TUZO ZA BODI BORA SEKTA YA BENKI NA BIMA

unnamed
Na Mwandishi Wetu,
MAKAMPUNI saba yamethibitisha ushiriki wao katika tuzo za bodi yenye uongozi bora katika sekta ya kibenki na bima zijulikanazo kama Best Board Leadership Awards (BBLA), zilizopangwa kufanyika Januari 30, mwakani katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mratibu wa tuzo hizo, Bi. Neema Gerald, imezitaja benki zilizothibitisha kushiriki katika tuzo hizo kuwa ni pamoja na Benki ya Posta (TPB), Benki ya Exim na Benki ya CRDB.
Aliyataja makampuni ya bima yaliyothibitisha kushiriki katika tuzo hizo kuwa ni Heritage Insurance, Alliance Insurance Corporation, Alliance Life Assurance na Strategis Insurance (T) Limited.
Tuzo hizo zimelenga kutambua uongozi bora wa Bodi za Wakurugenzi katika Sekta ya Kibenki na Bima.
Bi. Neema aliendelea kuzisihi kampuni zaidi zilizopo katika sekta ya kibenki na bima kujitokeza kwa wingi ili kujisajili katika tuzo hizo zilizoandaliwa chini ya mwamvuli wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) na Chama cha Makampuni ya Bima Tanzania (ATI).
“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa makampuni yaliyoonyesha mwamko wa kushiriki kwenye tuzo hizi katika hatua hizi za mwanzo za maandalizi,” alisema na kuongeza:
 “Tuzo hizi zitatoa fursa ya ufahamu wa jinsi gani bodi bora inaweza kusaidia taasisi kupata mafanikio na kufikia utendaji bora hususani katika eneo walilobobea kiutalaam. Hivyo ningependa kuziasa kampuni zaidi kujitokeza na kushiriki,” alisema Bi. Neema.
Alibainisha kuwa zoezi hilo, tathmini na upangaji wa mwisho wa matokeo utafanywa na jopo la majaji waliobobea na wenye rekodi bora za kiutendaji.
Tathmini hiyo italenga zaidi katika ufanisi wa Bodi ya Wakurugenzi katika suala la utawala wa taasisi, usimamizi wa fedha na uwezo wa kuiongoza dira ya taasisi kwa ujumla wake.
Maeneo mengine ni umakini wa bodi katika uwazi, uwajibikaji, utendaji, na ufuataji wa hatua madhubuti na  utendaji wake.
Alitaja maeneo mengine ambayo bodi itafanyiwa tathmini kuwa ni utoaji wa mitazamo yakinifu ya bodi katika kusisitiza umuhimu wa utendaji wa mtaji watu katika ngazi ya bodi na kuweka mbele vigezo vitakavyowezesha utendaji bora zaidi wa bodi, “alisema.
Bi. Neema aliwataja wadhamini wa tukio hilo la kipekee kuwa ni pamoja na Capital Plus Internaional Limited, Real PR Solutions Limited, Afrimax Strategic Partnerships Limited, Serena Hotel na IPP Media.
“Tumeona umuhimu wa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na wakurugenzi wa bodi katika taasisi zao.Tunaamini kuwa katika kila mafanikio ya taasisi ya kifedha, nyuma yake kuna bodi ya wakurugenzi imara na makini. Sasa, sifa hizo ambazo wajumbe wa bodi wengi wanakua nazo zinapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa, “alisema.
Bi. Neema alisema kuwa ni utamaduni uliozoeleka kwa Maafisa Watendaji Wakuu na Wakurugenzi Wakuu pekee kuthaminiwa na kutambuliwa na waajiriwa au jamii nzima kwa ujumla.
“Ni wakati muafaka sasa kwa bodi zenye utendaji bora kutambuliwa na kuzawadiwa kikamilifu kwa jitihada zao,” alisema.
Bi. Neema aliongeza kuwa tuzo hizo zimeanzishwa kwa wakati muafaka nchini kipindi ambapo sekta za Bima na kibenki zinapitia mabadiliko makubwa huku makampuni mengi zaidi ya bima yakijitokeza na masoko zaidi kuongezeka ili kufikia wateja wengi katika nyanja zote za maisha.
“Kwa mabadiliko haya yanayotokea wakati huu, hasa katika sekta ya fedha ambapo idadi kubwa ya makampuni ya bima na benki yamekuwa yakifungua biashara Tanzania, wateja wanahitaji kuwa na uhakika kuwa malipo yao ya bima yako salama na wanaweza kupatiwa kwa wakati wowote”, alisema.

No comments: