Friday, December 12, 2014

JK AMTEUA MAFURU NA WENGINE KUSHIKA NYADHIFA MBALIMBALI


Laurence Mafuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Laurence Nyasebwa Mafuru kuwa Msajili wa Hazina kuanzia tarehe 5 Novemba, 2014.
Taarifa iliyotolewa jana Desemba 11, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue inasema kuwa kabla ya uteuzi wake, Bwana Mafuru alikuwa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Fedha katika Ofisi ya Rais inayohusika na ufuatiliaji Miradi ya Matokeo Makubwa Sasa (PDB).  Aidha Bwana Mafuru pia alikuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya FBME iliyowekwa chini ya uangalizi wa muda wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).  
Wakati huohuo, Taarifa ya Balozi Sefue inasema Rais Kikwete amemteua Bibi Beng’i Mazana Issa kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuanzia tarehe 4 Desemba, 2014.  Kabla ya uteuzi wake, Bibi Mazana Issa alikuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Fedha katika Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS).
Rais pia amemteua Profesa Dominic M. Kambarage kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Kipya cha Kilimo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuanzia tarehe 5 Desemba, 2014. 
Taarifa hiyo ilisema kabla ya kuteuliwa kwake kuwa Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Kambarage alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro.
Taarifa ya Balozi Ombeni Sefue imesema kufuatia kuanzishwa kwa Chuo hicho kingine cha Umma, Rais Kikwete pia amemteua Profesa Lesakit S. Mellau kuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho upande wa Taaluma kuanzia tarehe 5 Desemba, 2014, na kabla ya uteuzi wake, Profesa Mellau pia alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro.
Aidha Taarifa ya Balozi Sefue imesema Rais Kikwete amemteua Profesa Msafiri M. Jackson kuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Kilimo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Utawala) kuanzia tarehe 5 Desemba, 2014.  Kabla ya uteuzi huo, Profesa Jackson alikuwa Mratibu wa Masomo ya Taaluma za Shahada za Juu katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam.

No comments: