
Na Mwandishi wetu, Arusha
TANZANIA imesema ipo tayari kuendeleza juhudi za kimataifa za kupunguza kuendelea kuliwa kwa tabaka la ozone kwa kuhakikisha kwamba inatunza misitu na kuwaelimisha wananchi juu ya menejimenti ya misitu hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira , Mh. Binilith Mahenge wakati wa kufungua kikao cha 13 cha wadau wanaotekeleza program ya kutunza misitu ya Umoja wa Mataifa REDD+ kinachofanyika Ngurdoto Jijini Arusha.
Alisema ingawa Tanzania kwa sasa ina hekta milioni 48.1 za misitu na mapori ambayo sawa ni asilimia 55 ya eneo lake, Tanzania kupitia misitu hiyo inanyonya zaidi ya tani milioni 76 za hewa ya ukaa ingawa yenyewe inatoa chini ya tani hizo.
Hata hivyo alisema kwamba pamoja na juhudi za serikali kuna changamoto kubwa katika kutunza misitu hiyo ambapo kiwango cha ukataji wa misitu kwa sasa ni kiasi hekta 372,000 kwa mwaka sawa na asilimia 1.1 ya eneo la ardhi la nchi.
Katika hali ya kawaida na endelevu eneo linaloruhusiwa kuvuna kwa mwaka linaweza kutoa mita za ujazo milioni 42.8 kwa mwaka wakati mahitaji halisi ni mita za ujazo Milioni 62.3 kwa mwaka.
“Asilimia 92 za mahitaji ni kwa ajili ya nishati kama kuni na mkaa.” Alisema akionesha changamoto zinazokabili serikali ya Tanzania pamoja na ukweli kuwa mabadiliko ya tabia nchi tayari yameonesha ukali wake nchini.

Mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na kuzidi kwa joto katika tabaka la ozone kumesababisha kupanda kwa bahari wka sentimeta 19 na kusababisha baadhi ya visiwa katika pwani ya Tanzania kuzama kama cha Maziwe kilichopo wilaya ya Pangani.
Aidha alisema keundelea kuyeyuka kwa barafu ni dalili nyingine ya Tanzania kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi kwa hiyo taifa la Tanzania linajikita pamoja na mataifa mengine kuhakikisha kwamba programu ya Umoja wa mataifa ya kuhifadhi misitu inafanikiwa.
Aidha alisema kwa mazingira ya sasa ambapo tani milioni 1 ya mkaa huzalishwa nchini kwa mwaka huu nusu yake ikitumika jiji la Dar es salaam na majiji ya Arusha na Mwanza yakitumia kiasi kinachobaki kunahitaji juhudi za ziada kuongeza kasi ya upandaji miti kiasi cha hekta 185,00 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 16 ijayo.
Waziri Binilith alisema pamoja na Tanzania na mataifa mengine ni laizma kushirikiana katika kupunguza kasi ya ukataji miti katika misitu huku wananchi wake wakisaidiwa njia nyingine ya kuendesha maisha yao.

Alisema mikakati ya kutunza misitu ili kupunguza kiwango cha joto duniani pia itasaidia kunyanyua uchumi wa wananchi, kuondoa umaskini na kutengeneza mtengamano wa mazingira na ekolojia hasa kwa jamii ambayo inategemea misitu kuwezesha maisha.
Waziri huyo aliwataka wadau waliopo katika mkutano huo wa siku mbili kujadili na kubadilishana uzoefu na kuhakikisha kwamba mkakati wa Umoja wa mataifa wa kukabiliana na mseleleko wa joto kwa kuwekeza katika kuhifadhi misitu unafanikiwa.
Umoja wa Mataifa una mpango wa kuhifadhi misitu unaojulikana kama Reduce Emissions from Deforestation and Forest Degradation (REDD+) unatarajia kuanza 2016-2020.
Wakati huo huo Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, akizungumza awali alishukuru mchango wa Norway katika kuwezesha utekelezaji wa programu ya UN REDD+ nchini Tanzania na maeneo mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa mkutanoni hapo Norway imechangia dola za Marekani milioni 11 kuwezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Umoja wa Mataifa katika kufanikisha programu hiyo katika nchi mbalimbali.

Utoaji wa hela hizo umeelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha kimataifa cha mabadiliko ya hali ya hewa katika Wizara ya hali ya hewa na mazingira ya Norway.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri Dk Binilith Mahenge, wawakilishi mbalimbali wa mashirika ya Umoja wa mataifa (– UNDP, UNEP, na FAO),Sekretarieti ya UN REDD, wajumbe wa bodi ya sera ya UN REDD, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Mwakilishi huyo wa UN alisema mafanikio yanayopatikana kwa sasa na duniani ni matokeo ya uwezeshaji wa Norway na wadau wengine katika mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuhifadhi misitu.
Alisema kazi ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha wanatoa msaada wa kitaalamu na misaada mingine kuiwezesha serikali kutimiza wajibu wake.
Alisema Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na nchi nyingine 56 duniani wanaounda UN-REDD wamefanya vyema kuziwezesha nchi hizo kuwa tayari katika kutekeleza programu husika kwa manufaa ya nchi zao na dunia kwa ujumla.

Alisema Tanzania kama nchi nyingine duniani zinazoendelea inakumbana na changamoto kubwa ya kuhifadhi misitu hasa kutokana na wananchi wake wengi kutegemea sana misitu kwa mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao.
Aidha alisema kama taifa lina uwezo mdogo wa kusimamia sera na sheria zinazohusu hifadhi ya misitu.
REDD+ ambayo imeanza kutekelezwa nchini Tanzania mwaka 2008, mikakati ya utekelezaji wa mkakati huo imefanywa na kupitishwa na Bunge la Tanzania mwaka 2013.
Kukiwa na kikosi kazi cha kuwezesha kutekeleza UN REDD+ Tanzania pia imepongezwa kwa kuanzisha miradi tisa yenye lengo la kuwezesha utekelezaji wa malengo ya REDD+
Aidha katika utekelezaji wake serikali imejikita katika vipato vingine kwa jamii inayoishi karibu au ndani ya misitu kwa kuwa na kilimo kinacholinda mazingira na ufugaji nyuki.

Alvaro alisema kutokana na mafanikio yaliyopatikana kwa sasa UN na serikali ya Tanzania wanakamilisha awamu ya pili ya UN REDD+ kwa kuangalia uzoefu uliopatikana katika awamu ya kwanza.
Utekelezaji wa awamu ya pili utafanyika mara tu fedha zitakapopatikana.
Naye Abbas Kitogo ambaye ni Meneja wa miradi ya nishati na mabadiliko ya tabia nchi (UNDP) alisema kwamba mkutano huo wa 13 utawezesha kubadilishana uzoefu wa sekta mbalimbali katika kutunza misitu huku wananchi wakiendelea kuneemeka.
Alisema nchini Tanzania kumekuwepo na miradi ya kujenga uelewa, kutengeneza mpango wa kutekeleza yanayotakiwa kufanywa na kujenga uwezo kwa wadau ili kujua REDD na kufuatilia athari za utekelezaji wa mradi huo.





No comments:
Post a Comment