MDEE ALAANI VURUGU ALIZOFANYIWA WARIOBA

Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), limelaani vikali vurugu alizofanyiwa aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, katika mdahalo wa kujadili Katiba inayopendekezwa jijini Dar es Salaam.
Pia, limewataka vijana wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) kutowavumilia watu wanaosadikiwa kumfanyia Warioba vurugu hizo wanaodaiwa kutoka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Maswa katika mkutano wa hadhara juzi, Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, alisema kitendo alichofanyiwa Jaji Warioba na wenzake kinatakiwa kulaaniwa na Watanzania wote.
Alisema ni jambo la kusikitisha na kufedhehesha sana kuona nchi inafikia hapo, kwa kumfanyia kitendo cha ajabu kiongozi mkubwa na mwadilifu kama yule ambaye amelitumikia taifa kwa moyo na nguvu zake zote.
“Jaji Warioba ambaye amefanya kazi nzuri katika taifa hili, leo hii anafanyiwa vitendo kama hivi, nchi hii inakwenda wapi jamanii, hatuwezi kuvumilia nchi iendeshwe namna hii, lazima hatua zichukuliwe,” alisema Mdee.

Comments