Thursday, March 13, 2014

WAENDESHA BODABODA, BAJAJI NA WAFANYABIASHARA MAENEO YASIYORUHUSIWA WANYOSHEWA KIDOLE, SASA KUKUMBWA NA OPARESHENI ENDELEVU YA KUWAONDOA

 Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna (CP) Suleiman Kova akitoa ufafanuzi ameeleza kwa waandishi wa habari kuhusu wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria za barabarani na kajenga tabia ya kufanya tathmini ya safari zao iwapo wanakidhi vigezo vya usalama barabarani ili kuepusha madhara.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki  akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kutoa agizo kwa viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanawaondoa na kuwachukulia hatua za kisheria wanaovunja sheria za jiji kwa kuendesha shughuli mbalimbali   katika maeneo yasiyoruhusiwa.

 Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Conrad Shio akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari  kuhusu sheria inayosimamia usafiri wa Bajaji na Bodaboda nchini.
---
 Na. Aron Msigwa –MAELEZO-Dar es salaam.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki amewaagiza viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanawaondoa na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani   wakazi wa jiji la Dar es salaam  wanaovunja sheriaa jiji kwa kuendesha shughuli mbalimbali   katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Aidha amewataka waendesha pikipiki  maarufu kwa jina la “Bodaboda”, Bajaji, waendesha baiskeli na mikokoteni wanaofanya biashara ya kubeba abiria na mizigo maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kuondoka wenyewe kabla hatua kali za kisheria hazijachuliwa dhidi yao.
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki amesema kuwa  jiji la Dar es salaam limeamua kuchuakua uamuzi huo kufuatia tatizo la baadhi ya wananchi kuamua kuvunja sheria zilizowekwa kwa kisingizio cha ugumu wa maisha na kutafuta fedha hali inayoleta usumbufu kwa wananchi wengine .
 
Amesema kuwa licha ya changamoto inayolikabili jiji la Dar es salaam hasa maeneo ya katikati ya mji hali iliyopo sasa ya biashara holela na uvunjifu wa sheria unaofanywa na maendesha Bodaboda, Bajaji, baiskeli, mikokoteni na Taxi bubu maeneo yasiyoruhusiwa kisheria hauwezi kuvumilika.
 
“Jiji la Dar es salaam tumekuwa na kero ya muda mrefu hasa ya omba omba, waendesha baiskeli, bodaboda na wafanyabiashara katika maeneo ya makutano ya barabara katika maeneo yasiyoruhusiwa hali hii hatuwezi kuivulimia, sisi hatufukuzi watu bali tunawataka wafuate sheria za jiji” Amesisitiza.
 
Ameeleza kuwa serikali haina lengo la kuwazuia wananchi kufanya biashara na shughuli nyingine za kujiingizia vipato kama wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na kuongeza kuwa wale wote wanaoomba leseni za kufanyia biashara wanapewa taratibu na miongozo na masharti ya kuzingatia wanapofanya biashara zao jambo ambalo wengi wao wanashindwa kulizingatia.
 
“Kila Manispaa ina miongozo na kanuni za uendeshaji wa shughuli zake ikiwa ni pamoja na mamlaka ya kutenga maeneo ya biashara na kuwaruhusu wale wanakidhi masharti ya leseni zao kufanya biashara zao ila wengi wao hasa madereva wa Bajaji na Bodaboda hawazingatii haya” Amesisitiza Mh. Sadiki.
 
Ameeleza kuwa sheria zote zilizotungwa zimewekwa ili zifuatwe kwa ustawi wa taifa na si vinginevyo na kubainisha kuwa wote waliovamia maeneo ya vituo vya mabasi, maeneo ya vituo vya umeme na hifadhi za barabara ni vema wakaondoka wenyewe na kukubali kutii sheria bila shuruti huku akitoa mfano wa baadhi ya wafanyabiashara na wauza vyakula “mama lishe” walio anza kuvamia maeneo ya ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo Kasi (DART).
 
“Haiwezekani sheria za jiji zikavunjwa na sisi tukaendelea kuwaangalia baadhi yao wamefikia hatua ya kuvamia maeneo ya mradi wa mabasi yaendayo kasi na kuanza kufanya biashara na kuwasumbua mafundi jambo lisilokubalika”
 
Akizungumza kuhusu biashara ya bodaboda inayofanywa na vijana walio wengi jijini Dar es salaam Mh. Sadiki ameeleza kuwa mpango wa serikali kuruhusu Bodaboda na Bajaji kutumika kubebea abiria ulikuwa na maana nzuri ya kuwawezesha wananchi kupata usafiri hasa katika maeneo yasiyofikika kirahisi kwa magari hasa vijijini na kuongeza kuwa utakua na mafanikio kama watafuata sheria.
 
‘Serikali iliruhusu usafiri wa Pikipiki na Bajaji kutumika kubebea abiria kwa nia nzuri ikiwa ni pamoja na kurahisisha usafiri na kuongeza ajira,hivyo siyo nia yetu kuwadhalilisha vijana hawa tunachowataka wafanye ni kufuata sheria za nchi”

Aidha kwa upande wa ongezeko la ombaomba ambao baadhi yao walirudishwa katika maeneo yao ya awali na kurejea tena jijini Dar es salaam ameeleza kuwa utaratibu wa kuwafuatilia uko pale pale na kufafanua kuwa watakaokutwa na makosa ya kukaa maeneo yasiyoruhusiwa watafikishwa mahakamani.
 
Kwa upande wake Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna (CP) Suleiman Kova ameeleza kuwa ni wakati sasa wa wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria na kusisitiza kuwa ni vema wananchi wakajenga mazoea ya kufanya tathmini ya safari zao iwapo wanakidhi vigezo vya kuwawezesha kutembea barabarani.
 
“Kwa waendesha pikipiki “bodaboda” hali ni mbaya wengi wameumia na kupata ulemavu wa kudumu kwa kutozingatia  sheria za usalama barabarani na kukidhi matakwa ya kuendesha pikipiki hizo”
 
Amesema kuwa Jeshi la Polisi litafanya kazi yake kwa kushirikiana na manispaa zote tatu kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa sheria vinakomeshwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona dalili zozote za uvunjifu wa amani hasa matukio ya ujambazi kwa kutumia pikipiki yayoendelea kuongezeka kwa kasi.
 
“Napenda niwahakikishie wananchi kuwa jeshi la polisi tumejipanga vizuri kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu wa aina zote, pia natoa wito kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam hasa wafanyabiashara kuepuka kutembea na fedha nyingi ili kuepuka madhara ya kuvamiwa”
 
Naye Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Conrad Shio ameeleza kuwa sheria ya usafirishaji kusimamia Bajaji na Bodaboda iko wazi na kuongeza kuwa serikali ina wajibu wake na pia waendesha pikipiki na Bajaji wanawajibu wao wa kuzingatia kanuni taratibu na kanuni zilizowekwa.
 
“Sisi kama SUMATRA tunaendelea kufanya kila tuwezalo kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjivu wa sheria za barabarani”

No comments: