Waziri Samia Suluhu Hassan Asema Muungano wa Tanzania umeendelea kuwa nyenzo na utambulisho muhimu katika kuleta umoja na maendeleo katika taifa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais( Muungano) Samia Suluhu Hassan akiongea na waandishi wa habari( Hawapo Pichani) kuhusu mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika utekelezaji wa masuala ya Muungano wakati wa Mkutano jana Mjini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Ofisi hiyo Bi. Siglinda Chipungaupi.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais( Muungano) Samia Suluhu Hassan jana mjini Dodoma.Picha na Hassan Silayo
---
Na Jovina Bujulu
Muungano wa Tanzania umeendelea kuwa nyenzo na utambulisho muhimu katika kuleta umoja na maendeleo katika taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mh. Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana mjini Dodoma.
“Miaka 50 ya Muungano imekuwa ni ya mafanikio makubwa ambayo yamewanufaisha wananchi katika nyaja mbalimbali kijamii, kiuchumi, na Kisiasa” alisema Waziri Suluhu.
Waziri Samia alisema kuwa muungano huo umeendelea kuwa kielelezo imara katika suala la ulinzi na usalama hali iliyowezesha kuwepo kwa amani na utulivu nchini.
Katika suala la haki za binadamu Waziri Samia alisema kuwa suala hilo limeendelea kupewa kipaumbele ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo wananchi wameendelea kupata haki zao za msingi kupitia mahakama za Mwanzo hadi za Juu.
Akifafanua kuhusu suala la elimu Waziri Samia alibainisha kuwa wanafunzi wenye sifa Tanzania Bara na Zanzibar wanapatiwa mikopo ili kukidhi gharama za Masomo, hali iliyosabisha uimarishwaji wa elimu ya juu kwani kuwekuwepo kwa ongezeko la vyuo vya elimu ya juu kutoka 25 mwaka 2015 hadi 63 vilivyopo sasa.
Aidha Waziri Samia alisema kuwa Serikali hizi mbili zinashirikiana katika kubuni na kuibua miradi ya Maendeleo inayofadhiliwa na Serikali kwa Kushirikiana na Wahisanai wa Maendeleo.
“Serikali hizi zimekuwa na ushirikiano wa pamoja katika masuala ya mandeleo mfano Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF III, MACEMP, ASDPL na ASDP kwa ujumla imekuwa ni chachu kubwa ya Maendeleo ya wananchi katika pande zote za Muungano” Alisema Waziri Samia.
Waziri Samia aliongeza kuwa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano yalizinduliwa Zanzibar tarehe 1 Machi na Rais wa Zanzibar Dkt. Ally Mohamed Shein ambapo nembo ya Muungano ilizinduliwa na sherehe za Muungano zitafanyika Dar es Salaam.
Kauli mbiu ya Mwaka huu ni “Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuumarishe na Kuudumisha.”
Comments