Monday, March 17, 2014

WAANDISHI WAHIMIZWA KUZINGATIA MAADILI KWENYE KURIPOTI BUNGE LA KATIBA

DSC_0641Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe Samia Sululu Hassan akifungua warsha ya siku moja kwa wahariri na waandishi wa habari juu ya nafasi ya watetezi wa Haki za Binadamu katika Katiba mpya.
.waambiwa waache kamari ya majongoo kuhusu serikali mbili ama tatu
.watetezi wa haki za binadamu, waandishi watoswa kwenye rasimu ya Katiba
Na Damas Makangale, Dodoma, MOblog
WAANDISHI na Wahariri wa vyombo vya habari nchini wamehimizwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na kuweka mbele maslahi ya taifa wakati wa kuripoti Bunge maalum la katiba. MOblog inaripoti.
Akifungua warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu nafasi ya watetezi wa haki za binadamu na asasi za kirai katika katiba mpya jijini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe Samia Sululu Hassan amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya haki za binadamu kupitia kalamu zao kwa kuzingatia weledi wa fani yao na maadili ya uandishi.
“waandishi wa habari pamoja na wahariri wao wanaweza kwa kuweka mbele maslahi ya taifa kuripoti na kuandika habari zenye kuleta suluhu, amani, mshikamano na utulivu,” amesema.
DSC_0650Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Ndg. Onesmo Olengurumwa akitoa mada juu ya ya mtazamo na jukumu la wabunge wa katiba na waandishi wa habari za katiba pamoja na watetezi wa haki za binadamu katika mchakato wa kuandika Katiba mpya mkutano wa siku moja uliofanyika mjini Dodoma.
Amesema waandishi wa habari kwa kutumia kalamu zao wanaweza kushauri na kushirikiana na serikali na mamlaka zingine kupatikana kwa katiba mpya yenye tunu za taifa,
Sululu aliongeza kwa kuweka hoja zao kwa ari ya utulivu wanaweza kabisa kuleta mshikamano na ushirikiano wa kitaifa katika kudumisha amani na haki za binadamu nchini.
Amesema kwamba kupitia bunge la katiba wanahabari ni kiungo muhimu katika kufikisha ujumbe kwa wananchi na kuelimisha umma jinsi sheria na haki za binadamu zinavyoweza kulinda na katiba ya nchi.
DSC_0627Mwezeshaji, Mwandishi wa Habari, Mwanasheria, msomi na mjumbe wa Bunge la Katiba Ali Uki akizungumza kwenye warsha hiyo.
“waandishi kwa kutumia nafasi yao wanaweza kushauri kwa kurekebishwa baadhi ya sheria, vifungu ili kuweza kulinda haki za binadamu nchini kwa kupitia bunge maalum la katiba,” aliongeza.
Alisisitiza Mhe Sululu kwamba bunge la katiba halijadili kuhusu ama serikali mbili au tatu kwa sababu kuna mambo mengi kwenye rasimu ya katiba yakujadiliwa.
“kwa jinsi mnavyoripoti kuhusu serikali mbili ama tatu ni kama mchezo wa kamari ya majongoo jamani katiba siyo muungano tu,” amesema.
Kwa upande, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo olengurumwa amesema ingawaje kwenye rasimu ya katiba hawajatambua watetezi wa haki za binadamu bali wataendelea kushauriana na wajumbe kupata mwafaka wa jambo hilo.
DSC_0629Meza kuu, Ndg. Onesmo Olengurumwa akiwa na Mgeni rasmi Samia Suluhu Hassani kwenye warsha hiyo.
“Rasimu ya katiba haijatambua mahali popote nafasi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki mbali mbali za raia kama zilivyoanishwa kikatiba,” amesema
Olengurumwa aliongeza kwamba rasimu ya katiba pia haijatambua wasaidizi wa kisheria wakujitolea (Paralegal) ambao wanatoa msaada mkubwa kisheria kwenye ngazi za vijijini.
Amesema ni muhimu kwa watanzania kuendelea kupanua mjadala wa katiba ili misingi ya haki za binadamu iingie kwenye mifumo ya utetezi wa haki za binadamu nchini.
Olengurumwa amesema waandishi wa habari kama vile watetezi wa haki za binadamu maisha yao lazima yalindwe na kutetewa na katiba ya nchi ili kujenga mazingira mazuri ya haki za binadamu nchini.
Hivi karibuni rasimu ya pili ya Katiba ilipendekeza Muungano wa Serikali tatu – Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanganyika.
Mjadala wake ulianza, ambapo wasomi walikosoa takwimu za Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu idadi ya waliotoa maoni, kuwa zimetumika kuupotosha umma.
wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sabato Nyamsenda na Bashiru Ally wakati wakizungumza katika kipindi cha Je, Tutafika? kinachorushwa na Channel Ten hivi karibuni.
DSC_0637Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo waandishi na wahariri kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Nyamsenda amesema ukweli wa takwimu hizo uko kwenye ripoti ya Tume hiyo, ambayo haipatikani kwa urahisi huku watu wakiishia tu kusoma tu rasimu ambayo haielezi majukumu waliyopewa, mahali walipopita, idadi ya wananchi na maoni yao.
Takwimu za Tume
Akifafanua zaidi, Nyamsenda anasema takwimu zinazotajwa kwamba asilimia 61 ya Watanzania Bara wanataka Serikali tatu, asilimia 60 ya Wazanzibari wanataka Serikali ya Mkataba si za kweli.
“Tume ya Warioba imetoa takwimu kuwa, watu waliotoa maoni kwa jumla ni 333,537. Kati yao, waliogusia Muungano ni 77,000, kwa hiyo 256,537 hawakugusia Muungano,” anasema na kuongeza:
“Ukiwagawanya katika Bara utakuta ni watu wapatao 36,000 na Visiwani watu 38,000. Kati ya waliozungumzia muungano. Kwa Zanzibar watu 19,000 hawakugusia muundo na watu 10,400 ndiyo waligusia Muungano wa Mkataba.”
Anaendelea kufafanua: “Waliozungumzia Serikali mbili ni 6,460 sawa na asilimia 34. Kwa hiyo ni wachache kuliko waliozungumzia Serikali ya Mkataba ambao nao ni wachache kuliko wale ambao hawakugusia kabisa suala la muungano. Ni sawa na tone la maji katika bahari,” amesema.
DSC_0656Benedict Ishabakaki, Afisa Usalama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu akishiriki mkutano huo.
Anaendelea kufafanua kuwa waliotoa maoni kuhusu Serikali ya Mkataba na Serikali tatu, ni wachache huku wengi wakiwa Bara.
“Kama jumla ya watu waliotoa maoni ya Katiba ni 333,537, huwezi ukachukua watu 16,000 waliotaka Serikali tatu ukawaziba wengi ambao hawakutaka,” anasema na kuongeza:
“Ukijumlisha watu wanaotaka Serikali moja na mbili ambao ni 16,475, utaona ni wengi kuliko wanaotaka Serikali tatu ambao ni 16,470.”
Anasema watu hao wakiwekwa katika kundi ambalo halikugusia kabisa muundo wa muungano, ni watu 287,537 sawa na asilimia 86.
DSC_0647Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha hiyo ya siku moja.

No comments: