Thursday, January 07, 2016

PROFESA MUHONGO AIOMBA NORWAY KUSAIDIA KUZALISHA WATAALAM WA GESI, MAFUTA

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimweleza jambo Balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad (kushoto) ofisini kwake mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.
Balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad, akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kabla ya kuanza kwa kikao hicho.
Balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad, akielezea uzoefu wa Norway kwenye sekta ya gesi na mafuta katika kikao chake na Waziriri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Kikao hicho pia kilihusisha watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na taasisi zake.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mbele katikati) akiongoza kikao kilichohusisha Balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad aliyeambatana na ujumbe wake, watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na taasisi zake.
Naibu Katibu Mkuu- Nishati, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) na Naibu Katibu Mkuu- Madini Prof. James Mdoe. (kushoto) wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad (hayupo pichani).
Naibu Katibu Mkuu- Nishati, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo akifafanua jambo katika kikao hicho.
Naibu Katibu Mkuu- Madini Prof. James Mdoe akielezea jambo katika kikao hicho.

……………………………………………………………………………………..

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospter Muhongo, ameiomba nchi ya Norway kuisaidia Tanzania kupitia mafunzo hususan katika utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta ili kuongeza wataalam wa gesi na mafuta nchini.

Profesa Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake na balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad aliyeambatana na ujumbe wake uliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam.

Kikao hicho pia kilishirikisha watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini ambao ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu- Nishati, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo, Naibu Katibu Mkuu- Madini Prof. James Mdoe.

Aidha, kikao hicho kilishirikisha watendaji kutoka katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ambazo ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA)

Profesa Muhongo alisema kuwa sekta mpya ya utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta inahitaji wataalam zaidi na kuongeza kuwa serikali imekuwa ikiwapeleka wataalam wake kwenda kusomea masuala ya gesi na mafuta katika vyuo vilivyoko nje ya nchi kama Scotland na Uingereza.

Alisema kuwa serikali imeanzisha kozi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Chuo cha Madini Dodoma.

“ Bado tuna uhitaji mkubwa wa wahadhiri wenye Shahada za Uzamifu (PhD) kwa ajili ya kufundisha katika vyuo vyetu, na kuzalisha wataalam watakaofanya kazi katika makampuni yanayojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini.

Akielezea kuhusu hali ya umeme nchini Profesa Muhongo alisema kuwa hali ya umeme nchini ni nzuri kutokana na serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika.

Alisema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imekuwa ikisambaza nishati ya umeme vijijini pamoja na kutoa ruzuku kwa wazalishaji umeme mdogo kwa njia ya maji (min-hydro) na kuitaka Norway kuisaidia REA ili iweze kufanikisha miradi yake.

Akielezea changamoto katika uzalishaji wa umeme nchini Profesa Muhongo alisema ipo mitambo ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji yenye kuhitaji matengenezo na kuiomba serikali ya Norway kusaidia matengenezo ya mitambo hiyo.

Aliongeza changamoto nyingine ni vyanzo vya maji kutosimamiwa ipasavyo katika mabwawa ya maji ya kuzalishia umeme na kusisitiza kuwa tayari serikali imeanza kufanyia kazi changamoto hiyo.

Naye Balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad alisema kuwa serikali ya Norway imekuwa na ushirikiano mzuri na serikali ya Tanzania katika sekta ya nishati na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.
Post a Comment