Monday, December 23, 2013

YANGA YAMTEMA RASMI BRANDTS, BIN KLEB AWEKA MAMBO HADHARANI LEO JANGWANI!!

binklebkatabaro (1)Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Abdallah Bin Kleb (katikati) akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu ya Yanga, kushoto ni Musa Katabaro na kulia Afisa Habari Baraka Kiziuguto. Picha kwa Hisani ya Young Africans Official Website
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
KIMENUKA jangwani!. Siku mbili tu baada ya Yanga kupata kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe, uongozi wa klabu hiyo umetangaza kuachana na kocha wake, Mholanzi, Ernie Brandts.
Mwenyekiti  wa Kamati ya Mashindano wa klabu ya Yanga Abdallah Bin Kleb amesema Uongozi umempatia taarifa (Notice) ya siku  thelathini (30) , Brandts juu ya kusitisha mkataba wake kuanzia jana Disemba 22 mwaka huu.
Bin Kleb amesema maamuzi hayo yanafuatia muenendo wa matokeo mabaya katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza la Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC mwishoni mwa wiki.
“Hatua ya Yanga kusitisha mkataba  na Brandts isichukuliwe kama chuki bali ni moja ya sehemu ya kuhakikisha tunaboresha benchi la ufundi ili tuweze kupata matokeo mazuri katika Mashindano yanayotukabili”. Alisema Bin Kleb.
 Bin kleb aliongeza kuwa Ukitazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga SC na wapinzani wao Simba Sc, na soka walilocheza kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe  ni dhahiri kocha amefikia mwisho kimbinu na hana njia mbadala.
“Yanga imekua ikicheza chini ya kiwango katika michezo ya Ligi Kuu hali iliyoplekea kupata ushindi kwa tabu na wakati mwingine timu kupoteza pointi”. Alisema Bin Kleb.
 Mwenyekiti huyo alisema kuwa Kufuatia kupewa taarifa ya siku 30, Brandts ataamua mwenyewe kama ataendelea kusimamia mazoezi ya timu au kuondoka moja kwa moja kabla ya muda huo ukiwa haujakamilika. 
Bin kleb aliongeza kuwa Ikiwa Brandts ataondoka mapema timu itaendelea na mazoezi kama kawaida  kila siku asubuhi katika uwanja wa bora kijitonyama kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa chini ya kocha msaidizi Fred Felix “Minziro”.
 “Ili kuhakikisha timuYanga  inafanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano ya kimataifa uongozi unakamilisha maandalizi ya safari ya kambi nje ya nchi na taratibu zote zitakapokamilika tutawajulisha”. Alisema Bin Kleb.
BRANDTSErnie Brandts amepewa `Notice` ya kusitishwa kwa mkataba wake.
Aidha uongozi upo katika mchakato wa kumapata mrithi wa Brandts ambaye ataungana na timu kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili na Mashindano ya klabu Bingwa Afrika.
 “Tunawaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa Yanga wasivunjike moyo kufuatia matokeo ya bonanza mwishoni mwa wiki, uongozi unajipanga kuhakikisha timu inaimarika kwenye benchi la ufundi na kurudisha furaha katika mzunguko wa pili wa VPL”. Alisema Bin Kleb.
Katika hatua nyingine , Bin Kleb amethibitisha ushiriki wa Yanga katika Kombe la Mapinduzi Januari mwakani visiwani Zanzibar.
Mwaka huu Yanga haikushiriki kombe la mapinduzi kufuatia kuwa na ziara nchini Uturuki ambako iliweka kambi ya wiki mbili.

No comments: