Friday, December 13, 2013

MASTAA WA SIKINDE KUSHUKA NA NYIMBO 5 TAMASHA LA GURUMO JUMAMOSI TCC CLUB

King Maluu na Yahaya wakipulkiza Saxophene
………………………………………………………………………………..
Komandoo kuibuka na 2, Mzee Makassy na Anifa wake
WANAMUZIKI nyota waliowahi kutamba na bendi ya DDC Mlimani Park “Sikinde Ngoma ya Ukae” watapiga bonge la show kwenye tamasha la Gurumo Jumamosi hii ndani ya TCC Club Chang’ombe.
Wakali hao ambao kwa sasa hawako na Sikinde, jana walihitimisha mazoezi ya nyimbo tano watakazopiga katika tamasha hilo.
Mazoezi hayo makali yalifanyika Amana Club ambako kwa wiki nzima wanamuziki watakaoshiriki tamasha hilo wamekuwa wakikutana hapo na kupiga mazoezi ya kufa mtu.
Baadhi ya nyimbo hizo ni pamoja na “Selina” utunzi wake Gurumo kwa kushirikiana na marehemu Joseph Mulenga, “Barua kutoka kwa Mama” uliotungwa na Cosmas Chidumule na “Gama” (Tshimanga Kalala Assossa).
Mratibu wa mazoezi hayo, Mzee Kassim Mapili alisema nyimbo mbili zingine za Sikinde zitajulikana siku ya onyesho lakini akafichua kuwa zitakuwa ni kati ya “Neema” (Chidumule), “Supu umeitia nazi” (Karama Legesu), “Nachechemea” na “Isaya” (Hussein Jumbe).
Wasanii waliowahi kuitumikia Sikinde ambao watakuwepo kumsindikiza Gurumo ni pamoja na Cosmas Chidumule, Abdallah Gama, Hussein Jumbe, Mashaka Shaaban, Kalamazoo, Henry Mkanyia na Karama Legesu. Wengine ni Ali Yahaya na Boniface Kachala, Tshimanga Kalala Assossa, Shaaban Lendi na Ibrahim Mwinchande.
Katika maendeleo mengine, Komandoo Hamza Kalala naye kwa kushirikiana na wakongwe hao, amekamilisha mazoezi ya nyimbo mbili “Vicky” na “Tumezaliwa wote Kijiji kimoja” ambazo zitapigwa Jumamosi kusindikiza tamasha hilo.
Mkongwe Mzee Makassy nae katika tamasha hilo atashuka na wimbo wake uliowahi kutamba sana “Anifa”.
Tamasha la Gurumo 53 ni maalum kwa ajili ya kuhitimisha miaka 53 ya utumishi uliotukuka katika muziki wa dansi kwa Muhidin Maalim Gurumo ambaye ametangaza rasmi kustaafu muziki.
Wasanii wengine wanaoshiriki mazoezi hayo ni Miraji Shakashia, Hafsa Kazinja, Juma Katundu, Edo Sanga Majengo na King Maluu.
Burudani zingine zitakazokuwepo siku hiyo ni pamoja na bendi za Msondo Ngoma Music Band, Talent Band, na Twanga Pepeta.

No comments: