Friday, December 06, 2013

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI ZANZIBAR YAFUNGUA KITUO CHA UTABIBU WA MIFUGO KASKAZINI B UNGUJA

 Waziri wa Fedha Zanzibar Mhe. Omar Yusuf Mzee akifungua pazia kuashiria ufunguzi wa kituo cha utabibu na uzalishaji mifugo kiliopo Mangapwani Mkoa Kaskazini `B’ Unguja.
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Kasim Gharib Juma akitoa maelezo  ya kituo cha utabibu na uzalishaji mifugo kiliopo Mangapwani Mkoa Kaskazini `B’ Unguja
 Waziri wa Fedha Zanzibar Mhe. Omar Yussuf Mzee akizungumza na  wananchi katika ufunguzi wa kituo cha utabibu na uzalishaji mifugo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Kasim Gharib na kushoto Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Pembe Juma Khamis.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika ufunguzi wa kituo cha utabibu na uzalishaji mifugo Mangapwani Mkoa Kaskazini `B’ Unguja wakimsikiliza Waziri wa Fedha Mh. Yussuf Omar Mzee( hayupo pichani).Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
--- 
Na Ali Issa na Miza Othman Maelezo –Zanzibar. 5/12/013
Waziri wa Fedha wa Zanzibar  Mh. Omar Yussuf Mzee ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwashajihisha wananchi wa Mangapwani na vitongoji vyake kukitumia kituo cha utababu na uzalishaji mifugo kilichopo Mangapwani Wilaya ya Kaskazini B  kupeleka mifugo yao kwa ajili ya  kupatiwa matibabu na kupata mbegu bora za mifugo.

Hayo ameyasema leo huko Mangapwani wakati wa uzinduzi wa kituo cha utabibu wa mifugo  kijijini hapo ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema  kwa muda mrefu wafugaji wamekua wakipata usumbufu wa kufuata huduma za mifugo mbali na eneo hilo  hivyo  utanuzi wa vituo vya utibabu na uzalisha mifugo  vijijini ni kuwapunguziamatatizo  wananchi  na amewashauri kuvitumia ili kuongeza uzalishaji wa mifugo.

“Ili kufikia lengo la kuwepo kwa kituo hiki hapa ni kwa wananchi kukitumia kikamilifu kupeleka mifugo yao kupatiwa matibabu, mbegu bora za mifugo na ushauri kutoka kwa watalamu wa mifugo”, alisema Waziri .

Aliongeza kuwa katika kufanikisha hatua hiyo   Wizara ya Mifugo italazimika kutoa elimu ya kutosha kwa wafugaji  kukitumia kituo hicho kupata matibabu ya  mifugo yao pamaoja na kupatiwa mbegu bora za kisasa za mifugo  itakayowapatia tija kwa haraka.

Alidokeza kuwa  kabla ya Mapinduzi ya 1964 kituo cha utabibu wa mifugo kilikuwa kimoja tu kwa Unguja  katika eneo la Maruhubi ambacho kilitoa huduma kwa wafugaji wote lakini kupelekwa huduma hiyo karibu na wananchi vijini ni frusa pana kwa wafugaji kuongeza uzalishaji. 

Nae Mkuu wa Mkoa  wa Kaskazini Unguja  Pembe Juma Khamiss akimkaribisha Waziri huyo  aliiomba Wiraza  pamoja na kituo hicho kujenga majosho ya kuoshea mifugo pamoja na kupeleka madaktari wa mifugo kituoni hapo.

Aidha alisema   hadi hivi sasa Mkoa wake umepata vituo viwili  vinavyotoa  huduma za Afya  ya mifugo  jambo linaloleta faraja kubwa kwa wananchi  kwani ndio mkoa unaoongoza kwa wafugaji wengi.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya  Mifugo na Uvuvi Kassim Gharibu amesema Wizara ya Uvuvi na Mifugo inawataalamu wakutosha wa afya ya mifugo jambo  ambalo  litawezesha vituo vyote vitakavyoanzishwa kutoa huduma kwa ufanisi bila matatizo yoyote.
Alisema  Wizara imejipanga vizuri kusambaza vituo vya huduma za mifugo   Unguja na Pemba na mpaka sasa imeshajenga vituo 23,  Unguja 12 na Pemba 11.

Ujenzi wa kituo hicho umefadhiliwa na Shirika la  Umoja wa Mataifa la IFAD na kimegharimu Shilingi milioni 22 za kitanzania.

No comments: