ISRAEL YAZINDUA SAFARI ZA KULETA WATALII KUJA TANZANIA , KUNDI LA KWANZA LAMALIZA ZIARA KWA MAFANIKO

Israel Photo 1Baadahi ya watalii kutoka Israel wakifanyiwa ukaguzi katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) kabla ya kupanda ndege kurejea kwao Isreal.
Israel Photo 2Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Safari company ya nchini, Israel Ronit Hershkovitz akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kuzindua safari ya kwanza ya watalii 150 kutoka Israel kuja moja kwa moja Tanzania kupitia shirika la Ndege la ELAL la nchini humo.
Na Geofrey Tengeneza
Kundi la watalii 150 kutoka Israel limemaliza ziara yake ya siku hapa nchini na kuondoka kurejea nyumbani kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro baada ya ziara yao waliyoilezea kuwa ni ya mafaniko makubwa.
Waisrael hao walifika nchini kwa ndege maalumu ya watalii ya shirika la ndege la Israel (ELAL) ambayo ilizianza rasmi safari zake za moja kwa moja kutoka Tel Avivi Israel kuja KIA Tanzania tarehe 29/11/2013. Miongoni mwa watalii hao walikuwemo watu kumi (10) wenye ulemavu wa aina mbalimbali, na wandishi wa habari saba (7) kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Israel yakiwemo magazeti maarufu,  kituo cha televisheni cha channel 10 ambacho ndiyo kikubwa nchini Israel na kituo cha televisheni cha channel 2. Watalii ishirini na wanne (24) kati ya hao 150 wakiwemo walemavu wote kumi, walikuja mahsusi kwa jili ya kupanda mlima Kilimanjaro huku wapiga picha wa televisheni ya channel 10 wakipiga picha tukio hilo la aina yake. Walemavu hao kumi walifanikiwa kupanda mlima Kilimanjaro hadi katika kituo cha Gilman. Watalii wengine waliosalia 126 walitembelea Hifadhi ya Taifa ya Manyara, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kreta ya Ngorongoro na baadae visiwa vya Zanzibar.
Akizungumza na wandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA, Mkurugenzi wa Kampuni ya utalii ya Safari Company ya nchini Israel iliyoratibu safari hiyo Bibi Ronit Hershkovitz amesema ziara hiyo pamoja na hatua ya shirika la ndege la Israel kuanzisha safari za moja kwa moja  kuja KIA kutafungua milango ya Tanzania kuanza kupokea idadi kubwa ya watalii kutoka Israel. Amesema ziara hiyo imekuwa ya kihistoria kwani wamefurahishwa sana  na upekee wa vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini “ndugu zangu wa Israel wamefurahia sana na kushangazwa na uzuri wa vivutio vya kitalii vya Tanzania. Kwa mfano makundi ya simba kule Serengeti, wanyama maarufu watano (the big five) na mlima Kilimanjaro vimewasisimua sana” alisema bibi Hershkovitz.
Naye Meneja Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) mkoani Arusha Bw. Willy Lyimo aliwashukuru watalii hao toka Israel kwa kuja kutembelea vivutio vya Tanzania na akawataka wakawe mabalozi wema wa Tanzania nchini kwao. “ Mmejionea kwa macho yenu na kukiri uzuri wa vivutio vyetu, tunaomba mkawaambie ndugu zetu waisrael kuwa tunawakaribisha sana, na tunapenda kuwahikishia kuwa Tanzania ni nchi salama kabisa na yenye amani tele” alisema Bw. Lyimo.
Safari maalumu za watalii (charter flights) za shirika la ndege la Israel zitafanyika kila juma ya mwezi April, Mei, Julai, Agosti, Septemba na Desemba, hii ikimaanisha kuwa kutakuwa na safari nne  kila mwezi uliotajwa hapo.

Comments