Monday, January 28, 2013

Breaking News:Lulu Apata Dhamana, arudishwa rumande



MSANII maarufu wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ amepata dhamana leo baada ya kukidhi masharti aliyowekewa na mahakama.
Dhamana hiyo imetolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam baada ya hoja za mawakili wanaomtetea kukubalika.
Masharti aliyokuwa amepewa ni pamoja na wadhamini wawili wafanyakazi wa serikali wenye kiasi cha Sh. milioni 20 kila mmoja na kuwasilisha pasi ya kusafiri ya msanii ili kutotoka nje ya nchi hadi kesi hiyo itakapokamilika.
Huku mashabiki wake na baadhi ya wasnii wenzake wakiwa na furaha mahakamani hapo, kila mmoja alisikika akisema Mungu mkubwa.

Habari zilizopatikana baadaye zikiandikwa naye
 
Happiness Katabazi zimeeleza kuwa
 
LICHA ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumpa dhamana msanii wa Filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, anayekabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba lakini amerudishwa rumande baada ya Msajili wa Mahakama kukosekana kukamilisha utarabu wa mtuhumiwa kuachiwa kwa dhamana.
Masharti hayo yaliyotolewa leo na Jaji Zainabu Mruke muda mfupi baada ya mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe kuiomba mahakama hiyo impatie dhamana mshtakiwa huyo ambaye anasota rumande tangu April mwaka jana ambapo walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha
148(1), (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
Jaji Mruke alisema ili mahakama impatie dhamana ni lazima asalimishe kwa Msajili wa Mahakama hiyo hati ya kusafiria, kutotoka nje ya Dar es Salaam  bila ruhusa ya Mahakama, kuripoti kwa msajili kila mwezi, kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali ambao watasaini bondi ya Sh. Milioni 20 kila mmoja.
Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo Lulu na wakili wake walitoka nje ya ukumbi uliokuwa ukiendeshwa kwa shauri hilo kwa ajili ya kwenda kwa msajili kutimiza masharti hayo lakini kwa bahati mbaya Msajili hakuwepo ofisini na hivyo kufanya Lulu kurudishwa rumande hadi kesho atakapoletwa kwaajili ya kujatimiza masharti hayo mbele ya Msajili wa mahakama hiyo.
Kufuatia mahakama hiyo leo kumpatia masharti ya dhamana Lulu kutoka na ombi lake Na.125/2012 la kuomba mahakama hiyo impatie dhamana, lakini bado kesi ya msingi inayomkabili Lulu ambayo ni ya kuua bila kukusudia bado haijapangiwa jaji wala tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Desemba 21 mwaka jana , Hakimu Mkazi Christine Mbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aliifunga kesi ya kuua bila kukusudia Lulu na kuiamishia rasmi kesi hiyo katika Mahakama Kuu, na uamuzi huo wa mahakama ulitokana na upande wa Jamhuri kumsomea maelezo ya kesi yake kwa kina mshtakiwa huyo na kuieleza mahakama kuwa wanakusudia kuleta jumla ya mashahidi tisa. 

No comments: