Serikali yalifufua Shirika la Reli


Rais Jakaya Mrisho Kikwete (yumo garini kushoto) akikagua sehemu ya kutua na kupaa ndege ya uwanja wa Tabora leo Januari 10, 2013 mara baada ya kuzindua rasmi ujenzi wake
Waziri wa Ujenzi Dkt John Pombe Magufuli (kulia)  na Waziri wa  Uchukuzi Dkt Harrison Mwakyembe wakiongea wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Tabora leo Januari 10, 2013


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe Radhia Msuya mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Kimataikfa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea mkoani Tabora alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku tano kukagua shughuli za maendeleo na kuzindua miradi mbalimbali
 (PICHA NA IKULU)
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
SERIKALI imetangaza hatua kubwa na kabambe za kufufua usafiri wa abiria na mizigo,  ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabehewa na injini za treni, katika hatua kubwa za aina yake kuchukuliwa na Serikali kwa muda mrefu katika kurekebisha usafiri wa treni nchini.
Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe ametangaza hatua hizo leo, Alhamisi, Januari 10, 2013, wakati alipokuwa anamkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka jiwe la msingi kwenye ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Tabora ikiwa ni tukio la mwisho la ziara yenye mafanikio makubwa ya siku tano ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete na mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uwekaji jiwe hilo la msingi kwenye Uwanja huo kuwa Wizara yake imeanza kubadilisha reli nyepesi, iliyochakaa na yenye uzito mdogo kwa Reli ya Kati.
Amesema kuwa kwa kupitia mashirika yake ya RAHCO na Shirika la Reli Tanzania (TRL) Serikali itafanya marekebisho hayo makubwa njia mzima ya Reli ya kati na kuwa mafundi wa mashirika hayo tayari wamefika Mkoa wa Morogoro.
Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa Serikali kupitia Wizara yake na mashirika yake hayo, imeagiza mabehewa mapya ya mizigo 274, imeagiza mabehewa mapya ya abiria 22, imeagiza mabehewa mapya ya kubebea kokoto 25 na pia imeagiza mabehewa ya breki (brake vans) 34 na tayari malipo ya awali yamefanyika.
Katika namna inayothibitisha dhamira ya Serikali kurekebisha hali ya usafiri wa reli nchini, Mheshimiwa Mwakyembe pia amewaambia wananchi kuwa Wizara yake pia imeagiza crane mpya na kubwa ya kubebea mizigo yenye uzito unaofikia kilo 100.
Kuhusu injini za treni, Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa zabuni kwa ajili ya kutengeneza upya (re-manufacturing) injini nane za treni imetolewa ili utengenezaji huo ufanyike, iwe ni ndani ama nje ya nchi.
Pia Waziri amesema kuwa oda imetolewa kwa ajili ya utengenezaji wa injini mpya 13 za treni ambazo malipo yake yatafanyika katika mwaka ujao wa fedha hata kama utengenezaji wa injini hizo utaanza.
Aidha, Waziri amesema kuwa Wizara kupitia mashirika yake hayo mawili imeagiza spea za kutosha kuweza kufanya ukarabati mkubwa wa injini tano kwenye karakana zilizoko hapa nchini.
“Mheshimiwa Rais, kwa hesabu nyepesi tu ni kwamba katika kipindi kifupi tutaweza kuwa na injini kiasi cha 26 ambazo zitarudisha uhai wa usafiri wetu wa reli kwa kiasi kikubwa sana,” Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete.
 Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
 10 Januari, 2013

Comments