Thursday, December 27, 2012

TAARIFA KUTOKA JWTZ KUHUSU MTU ALIYEJITAMBULISHA KUWA ASKARI JESHI KATIKA MKUTANO WA CHADEMA SIMANJIRO MKOANI MANYARA

 
Mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Monduli, Arusha akiwa na wabunge wa Chadema, Godbless Lema na Joshua Nassari baada ya kumaliza mkutano wa hadhara katika mji mdogo Mererani, Simanjiro mkoani Manyara.---

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeshitushwa na kusikitishwa kuona taarifa ya mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa JWTZ wa Kambi ya Monduli, Arusha, iliyochapishwa katika gazeti la Mwananchi la Desemba 24, 2012 akiwa amevaa sare za JWTZ.
Baada ya kuona habari hii JWTZ linafanya uchunguzi wa kina ili kutambua kama mtu huyo ni askari wa kweli au la. Kimsingi, JWTZ linafanya uchunguzi wa kumtambua mtu huyo kama kweli ni askari wake kwa sababu zifuatazo; kwanza Jina la mtu huyo halijaandikwa, pili kikosi halisi cha mtu huyo hakijaandikwa kwani eneo la Monduli lina vikosi vingi na hakuna kikosi kiitwacho Monduli.
Lakini pia inatia shaka kuwa mavazi yale siyo yale yanayotumika kwa wanajeshi wa JWTZ hivi sasa, kuna tofauti kati ya jampa (jacket) na suruali kama ilivyooneshwa katika picha hiyo.
Aidha, jampa la sare hiyo pia lina tofauti katika sehemu za mikono, jambo ambalo linatia shaka kama ni sare halisi ya JWTZ. Ilikuwa rahisi kumtambua mtu huyo kwa kuangalia uso, lakini mtu huyo anayedaiwa kuwa ni askari alifunika paji la uso ili asitambulike.
Pamoja na hali hiyo ilivyojitokeza, JWTZ linashughulika kumtambua mtu huyo kwa kutumia mbinu mbalimbali. JWTZ litakapobaini ukweli huo, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kutokana na Kanuni za Majeshi ya Ulinzi kwani, Sheria nambari nne (4) ya mabadiliko ya nane (8) katika Katiba ya Nchi ya mwaka 1992 ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha katika masuala ya kisiasa.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limesikitishwa kuchapishwa kwa picha hiyo kwani hakuna tija wala faida kwa wananchi wa Tanzania zaidi ya kuwatia hofu kuwa Vyombo vya Ulinzi navyo vinashabikia mambo ya siasa, wakati Katiba ya nchi imekataza jambo hilo.
JWTZ linawaomba wananchi waliangalie jambo hili kwa makini, kwa usalama wa nchi yetu.

 Imetolewana Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
 Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
 SLP 9203,
Simu: 0764 742161

1 comment: