Thursday, December 06, 2012

AZAM YAMUUZA NGASSA EL MEREIKH KWA MILIONI 120

AZAM FC imethibitisha kwenye tovuti yake leo kuwa imemuuza mchezaji wake Mrisho Halfan Ngasa kwa klabu ya El Mereikh ya Sudan kwa dola 75,000 (sawa na Sh. milioni 118) katika majadiliano yaliyochukua takriban saa moja kwenye makao makuu ya klabu ya Azam FC na kuhudhuriwa na viongozi wa pande zote mbili. Kwa mujibu wa Azam FC, El-Mereikh wameshazungumza na mchezaji na kukubaliana maslahi yake binafsi ambapo Mrisho Ngasa atalazimika kusafiri hadi mjini Khartoom, Sudan mara baada ya kuisha kwa mashindano ya CECAFA Challenge Cup ili kuona mazingira ya klabu, kufanya vipimo vya afya na kuangalia makazi yake binafsi. Kuuzwa kwa Mrisho Ngasa nchini Sudan kunaifanya klabu ya Azam FC kupata kiasi cha zaidi ya Dola 50,000 pesa ambayo Azam FC waliiweka kama kima cha chini cha kumuuza Mrisho Ngasa. Wakati Azam FC ikimtoa Ngasa iliweka kiasi hicho cha dola 50,000 kwa timu itakayomtaka lakini kutokana na kukosekana na mnunuzi huku Simba ikitoa ofa ya Sh. milioni 25, Azam FC iliamua kumpeleka Ngasa kwa mkopo Msimbazi ili akitokea mteja mwenye kufikia dau hilo waweze kumuuza. Mengi yalisemwa juu ya biashara ya mkopo kati ya Azam FC na Simba lakini msimamo wa Azam FC uliowekwa kwenye tovuti yao leo umethibitisha baada ya El-Mereikh kufikia dau la kumnunua Mrisho Ngasa. Mrisho Ngasa, mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu cha kusakata kabumbu anakwenda nchini Sudan kwenye kikosi chenye mafanikio zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati baada ya TP Mazembe. Azam FC inamuuza Mrisho Ngasa kwa kuzingatia umuhimu wa maendeleo ya mchezaji mwenyewe kimpira na kwa kipato, pia kwa kuzingatia kwamba Tanzania inahitaji wachezaji wengi wanaocheza nje kwenye vilabu vikubwa ili wanaporudi waweze kuisaidia timu ya Taifa. Taarifa zinasema Mrisho Ngassa mwenyewe amepewa dola 50,000 (sawa na Sh. milioni 79) kwa ajili ya kusaini na atalipwa mshahara wa dola 4,000 (sawa na Sh. milioni 6.3) kwa mwezi. Neema imeendelea kutua kwa Ngassa ambaye wakati alipouzwa na Yanga kwa Sh. milioni 58 kwa Azam FC Mei 2010 aliripotiwa kupewa mkononi Sh. milioni 40 na alipopelekwa kwa mkopo Simba Agosti 2012 alipewa gari aina ya Toyota Verosa pamoja na Sh. milioni 12 na sasa miezi minne tu baadaye ameweka kibindoni milioni 79.

No comments: