LULU AACHIWA KWA DHAMANA

Lulu katika siku za mwanzo za kesi yake, akifikishwa Mahakama ya Kisutu
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo asubuhi imemuachia kwa dhamana msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, anayetuhumiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba ‘The Great’ baada ya kupitia vifungu vya sheria.
Hatua hiyo inakuja baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kubadilisha mashitaka ya mwanadada huyo kutoka kesi ya mauaji hadi kuua bila kukusudia.
Kutokana na mabadiliko hayo, hata kama atashindwa kesi, Lulu hatapewa hukumu ya kunyongwa kwa kuwa anatuhumiwa kwa kesi ya kuua bila kukusudia na kwa mujibu wa kifungu cha sheria, anaweza kufungwa maisha au miaka kadhaa.
Lulu anakabiliwa na tuhuma za kumuua The Great Kanumba aliyefariki dunia, Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Vatican, Sinza Dar es Salaam.
Lulu aliyecheza filamu kadhaa na marehemu Kanumba waliyeibuka naye katika kundi la Kaole, Magomeni, anadaiwa alimsukuma Kanumba nyumbani kwake Sinza Vatican, ambaye pia inadaiwa alikuwa mpenzi wake.
Inaelezwa baada ya tukio hilo, Lulu alikimbia nyumbani kwa Kanumba na mdogo wa The Great, Sethi Bosco akaenda kuchukua gari kumpeleka kaka yake hospitali ya Muhimbili, ambako alipofika iligundulika amekwishafariki dunia.
Sethi alikaririwa akisema kwamba siku ya tukio, Lulu alikwenda kwao usiku wa manane na alipofika yeye (Sethi) alimuacha aongee na kaka yake. Sethi alidai aliwaacha sebuleni akaingia chumbani kwake na baadaye akasikia wameingia chumbani (kwa Kanumba).
Sethi alisema baada ya muda alisikia kelele za dalili ya ugomvi na baada ya muda Lulu alitoka kumwambia (Sethi) juu ya hali ya Kanumba kubadilika na kuwa mbaya.
Sethi alidai aliposikia hivyo akashituka na kwenda chumbani ambako alimkuta kaka yake katika hali mbaya, povu likimtoka mdomoni hivyo kuchukua hatua ya kumuita daktari wake, kabla ya kumkimbiza Muhimbili.
Lulu alikamatwa asubuhi ya kuamkia siku ya tukio hilo, linalodaiwa kutokea usiku wa manane na kuwekwa kizuizini katika kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni, Dar es Salaam, kabla ya kufikishwa mahakamani.
Uchunguzi wa madaktari katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ulisema pombe kali aina ya Jackie Daniels ilisababisha kifo cha mwigizaji huyo. 
Kifo cha Kanumba kiliwaumiza wengi, kwani msanii huyo alikuwa mahiri na kipenzi cha wapenzi wa filamu nchini.
Wapembuzi wa mambo wanasema huu ni msiba wa kwanza kuteka hisia za watu wengi zaidi, tangu kifo cha baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba mwaka 1999. Taarifa na picha za http://bongostaz.blogspot.com/

Comments