Thursday, July 10, 2008

Zitto alazwa


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akisumbuliwa na ugonjwa wa homa ya matumbo.

Akizungumza na Mwananchi jana jijini Dar es Salaam hospitalini hapo jana, Msaidizi wa Mbunge huyo, Omary Ilyas, alisema Kabwe alilazwa tangu juzi usiku katika jengo la Mwaisela, wodi namba nane, chumba 312 baada kuugua ghafla, lakini sasa anaendelea vizuri kufutia huduma kutoka kwa madaktari wa hospitali hiyo.

“Alifikishwa hapa saa tatu usiku wa kuamkia jana. Tunadhani tatizo lake linatokana na uchovu wa safari madaktari wake wameshachukua vipimo vyote, tunasubiri ni majibu na anaweza kuruhusiwa kwani kwa sasa anaendelea vizuri,” alisema Ilyas na kuongeza:

“Mheshimiwa Mbunge amekuwa na ziara mfululizo, bila kupata mapumziko kwa kipindi kirefu, hivyo inawezekana ndizo ziliyomsababishia maumivu makali ya mwili kiasi cha kumlazimu alazwe hapa kwa ajili ya mapumziko na uchunguzi zaidi”.

Aliongeza kuwa baada ya kufikishwa hospitalini hapo alipokelewa na jopo la madaktari bingwa na baada ya kupatiwa huduma ya kwanza walichukuwa vipimo mbalimbali kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusu matatizo aliyonayo.

Hata hivyo baadaye jioni, alipozumgumza Mwananchi Ilyas alisema madaktari wamegundua kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid), ambao umemsababishia homa kali na mwili kukosa nguvu.Imeandikwa na Jackson Odoyo na Saida Amini.

No comments: