SAKATA la utata katika mkataba wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) limechukua sura mpya baada ya kubainika kuwa mwekezaji amekwisha kuanza kazi, wakati viongozi wa CCM wakidai kwamba mkataba haujasainiwa.
Wakati Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Francis Isaac, anasema kuwa vifaa vya ujenzi vimekwisha kuwasili kwenye eneo la ujenzi kama sehemu ya matayarisho, Mwananchi imeshuhudia ujenzi halisi ukiwa umekwisha kuanza.
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba licha ya juzi kusema kwamba mkataba huo haujasainiwa, jana alishindwa kueleza sababu za mwekezaji huyo kusogeza vifaa eneo la ujenzi akisema kuwa hahusiki na masuala ya ujenzi, ila mkataba ambao ameona kuwa unafaa.
Makamba aliliambia gazeti hili kuwa mkataba huo una manufaa kwa UVCCM ila hawezi kuzungumzia suala la mwekezaji huyo kusogeza vifaa kabla ya kusainiwa kwa mkataba huo kwani halimhusu.
"Mimi ninachosema mkataba huo una manufaa kwa UVCCM, kuanza ujenzi ni suala lingine ambalo mimi sihusiki nalo unaweza kuwapigia wenyewe (UVCCM) waseme kwa nini mwekezaji huyo amesogeza vifaa wakati mkataba haujasainiwa," alisema Makamba na kuongeza:
Ujenzi ni suala la kiufundi, linahitaji vibali na kuthibitishwa na mamlaka mbalimbali siwezi kuzungumzia hilo na ukitaka waulize wenyewe watoe majibu,"Habari ya Kizitto Noya
Comments