Tuesday, July 15, 2008

Kivumbi chaanza UVCCM



KADA wa Chama Cha Mapinduzi Nape Nnauye na mgombea uenyekiti wa UVCCM taifa, amechukua fomu leo ya kugombea uenyekiti wa umoja huo taifa.

Akizungumzia kuhusu uamuzi wake wa kugombea nafasi ya mwenyekiti wa UVCCM, Nnauye alisema amelenga kukabiliana na changamoto kadhaa zinazoukabili umoja huo ikiwamo kushindwa kwake kubadilika kuendana na matakwa ya nyakati.

Alisema UVCCM ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitetea wanyonge, imeshindwa kushughulikia matatizo ya vijana kwa kukemea ufisadi jambo alilosema kuwa linahitaji kiongozi madhubuti kulifanya.

"Vijana ndio waliotembea katika Azimio la Arusha kuwafukuza mabeberu lakini leo wakati jamii inazungumzia ufisadi, UVCCM inakaa kimya!," alishangaa.

Alisema vita dhidi ya ufisadi ni ngumu na inahitaji nguvu za pamoja za vijana kupambana nayo hivyo sio sahihi kwa UVCCM yenye kazi ya kuwapika viongozi kimaadili kutoizungumzia.

Alisema mbali na changamoto hiyo UVCCM imeshindwa kuhifadhi na kutunza vyanzo vyake vya mapato pamoja na kutafuta miradi mbadala ya mapato kukabiliana na hali ngumu ya uchumi.

"... Kisiasa UVCCM imeshindwa kuweka mikakati ya kupata wanachama wapya na kudhibiti wanachama waliopo, pia imeshindwa kuhifadhi vyanzo vyake vya mapato na kwenda sambamba na mahitaji ya mabadiliko ya nyakati," alisema.

Kwa mujibu wa Nnauye UVCCM imeshindwa kubadilika na kukidhi mahitaji ya mfumo wa siasa wa vyama vingi badala yake imeendelee kung'anga'nia siasa za mfumo wa chama kimoja jambo ambalo ni hatari kwa uhai wake na chama.

"Moja ya kazi za UVCCM ni kuwa tanuru la kupika viongozi lakini hakuna mikakati yoyote ya kuongeza wanachama, kukemea ufisadi na kutengeneza vyanzo mbadala vya mapato," alisema. Habari na Kizitto Noya.

1 comment:

Anonymous said...

eehhh bwana nimekuwa nikifuatilia hili suala kwa uhakika hawa kina makamba na wenzao nakuambia kaka wanamfa Nnape free ride na sasa wanampaisha sijui kwa kutokujua au ni kwa makusudi, kilichofanyika katika jengo la Umoja wa Vijana pale barabara ya Morogoro ni aibu, huraa endelea kutupa vituuuz.