Hussein Bashe achukua fomu uenyekiti UVCCM


MWANASIASA chipukizi na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Bashe, amejitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Bashe ambaye jana alifika makao makuu ya umoja huo jijini Dar es Salaam kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo, alisema nia yake ni kuipanga upya jumuiya hiyo ili kuondokana na changamoto za kikanuni na mifumo.

"Ingawa UVCCM imejitahidi kutekeleza majukumu yake mengi kwa ufanisi, bado naona kuna changamoto nyingi, bado Jumuiya inapaswa kujipanga na kujitazama upya ili iweze kukidhi mahitaji na matarajio ya vijana wa Kitanzania kwa nyakati za sasa," alisema.

Katika waraka wake kwa wanaUVCCM, Bashe alisema akichaguliwa kushika wadhifa huo, atafanya mabadiliko ya msingi katika jumuiya hiyo ikiwamo kuifanya Jumuiya hiyo kuwa jukwaa la vijana kutoa mawazo yao.

Alisema pia atatumia fursa hiyo kubadili muundo wa utawala na kalenda ya vikao, kuanzisha kamati ya maadili, kuipa uhai idara ya chipukizi na uhamasishaji, kuifanya jumuiya kuweza kujitegemea kiuchumi na kuanzisha Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) kwa ajili ya vijana.

Alisema pia atadhibiti uhamisho wa viongozi usio wa lazima, kuboresha maslahi yia watendaji, kuanzisha utaratibu wa kuwapatia posho wenyeviti na kuanzisha utaratibu wa kukutana na makatibu ambao ni watendaji wa chama. Habari ya Kizitto Noya na picha ya Mpoki Bukuku.

Comments