MWANDISHI wa habari wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, Esther Katua (pichani), amefariki dunia.
Esther alifariki katika hospitali ya Lugalo Dar es Salaam jana, alikokuwa amelazwa kwa matibabu baada ya hali yake kuwa mbaya.
Alifikishwa hospitalini hapo Jumatatu ya wiki hii baada ya kuzidiwa alipokuwa
akijiuguza nyumbani kwao Ilala, Dar es Salaam.
Kifo cha mwanahabari huyo kimetokea siku ambayo pia alichaguliwa kuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Tawi la Uhuru na mjumbe wa UWT wa tawi kuwakilisha vijana.
Wakati wa uhai wake, mbali ya magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Esther aliwahi
kuandikia magazeti ya ZanzibarLeo na Mwananchi. Esther alijiunga na magazeti ya Uhuru katikati ya miaka ya 1990.
Kwa waliomfahamu Esther wakati wa uhai wake, alikuwa ni mkarimu, mchapakazi hodari, mchangamfu na aliyependa kushirikiana na watu katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Hadi jana jioni ilikuwa haijafahamika maziko ya marehemu Esther yatafanyika lini na wapi.
Comments