Tuesday, May 27, 2008

Kesi ya Zombe yaanza kunguruma Mahakama Kuu



KESI ya mauaji kukusudia inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Abdallah Zombe na wenzake 12, imeanza kusikilizwa jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania na mashahidi 50 upande wa mashitaka wanatarajia kutoa ushahidi.

Kesi hiyo ambayo ilivuta umati mkubwa wa watu, ambao walifika katika mahakama hiyo ili kuisikiliza, ilianza saa 4.15 asubuhi mbele ya Jaji Salum Masatti wa mahakama hiyo.

Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani, alikuwa Mathew Alex Ngonyani, ambaye alieleza mahakama kuwa alipata taarifa za kukamatwa na kuuawa kwa wafanyabiashara hao, wakati akiwa kwenye machimbo ya madini huko Mahenge, ambao walikwenda kuuza madini Arusha na Dar es Salaam.

Alisema mwishoni mwa Desemba mwaka 2005, marehemu Sabinus Chigumbi maarufu kama Jongo, alipata madini na kumwomba Ngonyani amsindikize kwenda kuyauza, Dar es Salaam au Arusha.

Alisema kabla ya kuondoka Mahenge, walipata taarifa kuwa wakaguzi wa migodi wangefika kukagua migodi hiyo, hivyo wakaamua kubaki ili kuwasubiri wakaguzi hao.

Alifafhamisha kuwa Marehemu Jongo aliondoka pamoja na Ephraimu Chigumbi, Mathias Lugombi na Protas Mchami wakiwa wanaendesha gari ya Jongo aina ya Landcruser Prado, kwenda Dar es Salaam na baadaye kuelekea Arusha, ambako waliuza madini kidogo kutokana na soko kuwa baya na mengine waliyauza Dar es Salaam.

Ngonyani alidai kuwa wakiwa Dar es Salaam walifikia katika Hotel ya Bondeni, iliyoko Magomeni na kwamba kabla ya kuondoka aliwaagiza wafike nyumbani kwake Sinza Palestina ili kumsalimia mkewe na kumpa fedha za matumizi. Imeandikwa na James Magai

2 comments:

Egidio Ndabagoye said...

Kaikosea nini CCM mzee Zombe?

Anonymous said...

huyu hana rafiki ndani ya chama angeshatoka