Wednesday, May 28, 2008

Mama wa Ballali awekwa chini ya ulinzi mkali

MAMA wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Ballali amewekwa chini ya ulinzi katika nyumba ya mtoto wake iliyopo Boko, wilayani Kinondoni, nje kidogo ya Jiji la Dares Salam.

Ulinzi huo ambao umewekwa kwa wiki nzima tangu kutokea taarifa za kifo cha Ballali kwa maelekezo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), unazuia watu mbalimbali kuingia, wakiwemo waandishi ili wasikutana na mama huyo wala yeye kuzungumza chochote.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema benki hiyo haijatoa maelekezo ya kuwepo ulinzi nyumbani kwa mama huyo.

"BoT haijatoa maelekezo ya kuwepo ulinzi, kwa nini itoe maelekezo ya kuwepo ulinzi, au kwa nini iingilie mambo ya familia?" alihoji Profesa Ndulu.

Kwa mujibu wa profesa Ndulu, BoT imekuwa ikiwezesha kufanyika mambo manne ambayo ni ubani, viti, mahema na vinywaji.

"Inachofanya BoT ni kusaidia matanga kwa vitu vinne, ambavyo ni ubani, viti, mahema na vinywaji, lakini hayo mambo ya ulinzi hatuyajui," alisisitiza.
Gavana Profesa Ndulu aliongeza kwamba, suala la ulinzi katika nyumba hiyo ni la familia.

Alifahamisha kuwa ulinzi katika nyumba hiyo ulikuwepo kabla ya matanga na kutaka watu wasiitwishe BoT mzigo ambao si wake.

Profesa Ndulu alifafanua kwamba, BoT itaendelea kusaidia familia hiyo hadi itakaposema kwamba matanga yamekwisha.

"Jamani, msiivishe BoT gunia la moto, sisi hatuhusiani na hayo mambo ya ulinzi, ila tunasaidia na tutaendelea kusaidia matanga hadi familia itakaposema imemamiliza matanga," alisema. habari ya Ramadhan Semtawa wa Mwananchi.

2 comments:

Anonymous said...

Labda tukumbushane Kiswahili fasaha.Kuwekwa chini ya ulinzi ni kukamatwa baada ya kuvunja sheria ,kanuni au taratibu.Mama yake marehemu Balali kawekewa ulinzi sio kawekwa chini ya ulinzi.

Anonymous said...

kama familia imesema asiseme chochote basi, ila kama ni watu flani kwa sababu zao binafsi wanamshinikiza asiseme watakuwa hawamtendei haki.bibi wa watu ana uchungu sana jamani, mtoto kwa mzazi hakui hata siku moja na uchungu wa mwana aujue mzazi haswa mama. Mungu aendelee kumfariji bibi wa watu.