Friday, May 23, 2008

IGP atibua safu ya jeshi

JESHI la Polisi nchini limefanya mabadiliko makubwa ya uongozi, ambayo yamefanya Kamanda wa Polisi Mbeya, Suleiman Kova kuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Alfred Tibaigana aliyestaafu.

Kamishna Tibaigana, ambaye atastaafu rasmi Julai, mawaka huu ni wa kwanza kuongoza Kanda Maalum ya Dar es Salaam baada ya Jeshi la Polisi baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuanzisha kuzifanya wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke kuwa mikoa katika operesheni za polisi .

Mabadiliko hayo ambayo yameacha furaha na majonzi kwa baadhi ya maafisa wa jesh hilo, yanagusa nafasi za makamanda wa polisi mikoa (ma-RPC), Wilaya (Ma-OCD) na Wakuu wa Upelelezi (Ma-RCO) na wengine walio katika nafasi mbalimbali.

Kufanyika kwa mabadiliko hayo kunatokana na kujaza nafasi za maafisa ambao wanastaafu akiwemo Kamishna Tibaigana, ambaye amestaafu baada ya kutimiza umri wa miaka 60.

Pamoja na Tibaigana, askari wa ngazi za chini 700 ambao kwa pamoja watatimiza miaka 55 wamestaafu, huku maafisa wengine wakirudishwa makao makuu, ifikapo Julai mosi, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Jeshi hilo, Clodwig Mtweve alisema nafasi ya Kamanda Kova itachukuliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Zelothe Stephen.

Kwa mujibu wa Mtweve, katika mabadiliko hayo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Jamal Rwambo anakwenda Mwanza kuchukua nafasi ya Stephen.

Mtweve alifafanua kwamba, Mamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi (ACP) David Saibullu anastaafu na nafasi yake itachukuliwa na Kamishna Msaidizi (ACP) Leberatus Barlow ambaye alikuwa ni Afisa Nadhimu, Utawala na Fedha wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Nafasi ya ACP Rwambow itachukuliwa na Kamishna Msaidizi ( ACP) Mark Kalunguyeye kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, huku Kamishna Msaidizi (ACP) Ray Karama, kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akiteuliwa kuwa Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo ambako Makao Makuu yake yako Arusha.

Katika mabadiliko hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Kamishna Msaidizi (ACP) Abdallah Msika anarejeshwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, ambako haikuelezwa atafanyakazi gani huku nafasi yake ikichukuliwa na Kamishna Msaidizi (ACP) Selewi kutoka Mkoa wa Pwani.

Kamishna Msaidizi (ACP) A, Mwakyomba kutoka Makao Makuu anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi (ACP) M. Msafiri analetwa Makao Makuu ya
Kurugenzi ya Upelelezi (CID).

No comments: