VIONGOZI wa vyama vya upinzani wamepinga kauli zilizotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu dhamira ya serikali kukabiliana na ufisadi wakisema kuwa kauli hizo ni hewa na hazina uzito wa kuuma mafisadi.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema amesema serikali inafanya kiini macho katika kushughulikia suala la ufisadi na kwamba kauli aliyoitoa Waziri Pinda wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari juzi inaonyesha ni jinsi gaini imeshindwa kukabiliana na tatizo hilo na haipo makini.
Akizungumza na Mwananchi jana katika mahojiano maalumu, Mwenyekiti huyo wa TLP alisema kuwa Waziri Pinda si mkweli kwa sababu tangu amechaguliwa hajafanya chochote kukabiliana na ufisadi nchini licha ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mchakato mzima wa kutoa kwa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond ya Marekani kutoa mapendekezo yake.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic (UDP), amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwakemea viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi, akiwamo Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, kuacha kuwatumia wananchi majimboni mwao kuwatukuza kama mashujaa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alipozungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana.
Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), alisema kitendo hicho licha ya kuwa ni kinyume na utamaduni wa Kiafrika, ni cha aibu kufanywa na mtu aliyetuhumiwa kwa ufisadi. Habari na Tausi Mbowe na Muhibu Said.
Comments