Sherehe za May Mosi Dar








WAFANYAKAZI wametaka jitihada za kupambana na ufisadi zikafanyika kwa kasi kubwa kwa lengo la kupunguza makali ya maisha yanayowakabili wananchi wenye kipato cha chini.

Akisoma Risala ya wafanyakazi kwenye sherehe za maadhimisho ya Mei mosi zilizofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Katibu wa TUCTA Everest Mwalongo alisema kuwa Mtandao wa ufisadi umeendelea kuongezeka na kuifanya Serikali kushindwa kumudu kufanya shughuli za kimaendeleo.

Alisema wafanyakazi wanaamini kuwa kama kusingekuwa na mafisadi serikali ingekuwa na uwezo mkubwa kwa kuihudumia jamii kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara na marupurupu mazuri kwa watumishi wake kulingana na mfumuko wa bei za bidhaa uliopo.

"Tunaomba kuieleza Serikali kuwa viongozi wengi mafisadi katika serikali yetu bado hawajafikiwa hivyo tunamuomba Rais Jakaya Kikwete aache kuwaonea haya na tunamthibitishia kuwa sisi tuko nyuma yake kumuunga mkono,"alisema Mwalongo.

Mwalongo alisema mtindo wa serikali kuongeza mishahara kwa kuzima moto kwa makundi madogo madogo kadri yanavyojitokeza kwenye maandamano, yanaweza kuleta athari baadaya kwani watumishi wanakuwa wanatofautiana kwa miundo ya mishahara kupita kiasi.

Alisema hali hiyo inatoa sura ya upendeleo kwamba wengine wanafaa na wengine hawafai,kitu ambacho kinaweza kuleta matokeo mabaya ya kuporomoka kwa tija na ufanisi na maadili mema katika kazi. Habari hii ya Peter Edson wa Mwananchi, Picha zote za Kassim Mbarouk.

Comments