Thursday, January 07, 2016

SERIKALI YAANZA KUTUMIA MFUMO WA SIMU ZA MKONONI KUWAWEZESHA WAMILIKI WA ARDHI KUHAKIKI NA KUBORESHA TAARIFA ZAO

Msemaji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Mboza Luandiko akifafanua kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu namna mfumo mpya wa kuhakiki taarifa za umiliki wa viwanja na mashamba kwa kutumia simu za mkononi utakakavyofanya kazi na kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi hapa nchini,kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TEHAMA Bw.Alexander Karaba.

Frank Mvungi

Serikali yaanza kutumia mfumo wa simu za mkononi kuwawezesha wamiliki wa ardhi kuhakiki na kuboresha taarifa zao za ardhi kote nchini.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Msemaji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Mboza Luandiko wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kutambulisha huduma hiyo mpya kwa wananchi.

“Mfumo huu unamwezesha mmiliki wa ardhi kuhakiki na kuboresha taarifa zake za ardhi kwa kutumia simu yake ya mkononi kwa kuandika neno Ardhi kwenda namba 15774” alisisitiza Luandiko

Akifafanua Luandiko amesema kuwa wakati mwananchi anatuma ujumbe huo anatakiwa awea na nyaraka zake za umiliki wa ardhi au barua ya toleo kwa wale ambao bado hawajapata hati.Akizungumzia faida za mfumo huo Luandiko amebainisha kuwa utasaidia kulinda milki za wateja na kuondoa kabisa tatizo la matapeli.

Faida nyingine ni kuongeza uwazi katika kugawa ardhi na hivyo kupunguza migogoro ya ardhi ambapo hati milki zitatolewa kwa wingi zaidi kwa kuwa mfumo huo ni rafiki katika utoaji wa huduma.

Aidha mfumo huu utarahisisha Mawasiliano kati ya mmiliki wa ardhi na Wizara hali itakayoongeza tija katika upatikanaji wa huduma kwa kuwa zinaweza kupatikana kwa njia ya simu ya mkononi ikilinganishwa na hapo awali ambapo mwananchi alitakiwa kufika katika Ofisi za Wizara ili kupata huduma husika.

Huduma ya mfumo wa uhakiki wa taarifa za umiliki wa viwanja na mashamba imeanza katika mkoa wa Dar es salaam na baada ya hapo tathmini itafanyika kabla ya kuanza kutumika katika Mikoa yote
Post a Comment