Wanafunzi Temeke wafunga barabara



ZAIDI ya wanafunzi 1000 wa shule za msingi za Umoja na Miburani zilizoko Temeke Dar es Salaam, jana walifunga barabara kwa zaidi ya saa nne na kusababisha vurugu kubwa katika eneo la Sudani, makutano ya Barabara ya Tandika na Temeke.

Huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa kutaka eneo hilo liwekewe matuta, wanafunzi hao waliokuwa na silaha mbalimbali, walirusha mawe hovyo na wengine kurukaruka barabarani.

Vurugu hizo pamoja na zile za kurushia mchanga magari, zilisababisha msongamano mkubwa wa magari katika eneo hilo.

Habari zilizosema fujo hizo zilitokana na mmoja wa wanafunzi hao kugongwa na daladala.

Kwa mujibu wa habari hizo, tukio hilo ni la tatu kutokea katika eneo hilo. Juzi mwanafunzi mmoja alinusurika kugongwa na gari na mwingine aligongwa na guta.

“Hatutoki hapa mpaka matuta yajengwe leo, serikali mbona mnatuua, Jengeni matuta basi, hapa hakieleweki tunataka haki yetu.” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

“Tumeenda wilayani eti wanatuambia turudi shuleni watakuja kujenga matuta baada ya siku tatu lakini, sisi bado tunakuja shule na kuvuka barabara hii, hatudanganyiki,” alisema mwingine.

Mashuhuda wa tukio hilo walilieleza gazeti hili kuwa saa 1:00 asubuhi ya jana, mwanafunzi Abdul Idrisa wa darasa la pili katika Shule Msingi Umoja, aligongwa na daladala iliyokuwa inatoka Tandika kuelekea Kariakoo.

Mwanafunzi huyo alipata majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili na kukimbizwa katika Hospitali ya Temeke kwa matibabu.

Hata hivyo Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk Gilbert Buberwa, alisema hali ya mwanafunzi huyo inaendelea vizuri.

“Tulimpokea mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka saba, saa 3:00 asubuhi na baada ya kumfanyia X-ray, tumegundua kuwa amejeruhiwa maeneo ya miguuni lakini, uchunguzi bado unaendelea," alisema Dk Buberwa na kuongeza; Habari imeandikwa na Felix Mwagara: SOURCE: MWANANCHI

Comments