Wednesday, February 17, 2010

Maunga adakwa na dawa za kulevya



HALID Salim Maunga (35), raia wa Uingereza aliyekuwa na hati ya kusafiria namba 109483453, juzi asubuhi alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kete 69 za madawa ya kulevya aina ya cocaine pamoja na bangi gramu 610.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamishna Msaidizi wa Polisi wa viwanja vya ndege nchini, Mwajuma Kiponza alisema Halid alikamatwa na askari wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya viwanja vya Ndege (TAA) wakati akiwa katika hatua za mwisho za ukaguzi katika uwanja hapo.

Alisema polisi pamoja na maofisa hao, walimtilia mashaka raia huyo, wa Uingereza aliyekuwa amefikia maeneo ya Makumbusho jijini Dar es Salaam na kuanza kumpekua na walibaini alificha kete 16 kwenye pindo la suruali yake sehemu ya kiunoni na kete 14 zilikutwa katika pindo ya chini ya suruali yake.

“Baada ya kumgundua kuwa amebeba vitu hivi polisi walimkamata na kumpeleka kituoni kwa ajili ya kumhoji zaidi, lakini walipofungua begi lake walikuta vinyago vitatu ambavyo vilikuwa na kete hizo za madawa ya kulevya pamoja na bangi.

“Vinyago hivyo vilikuwa na mfano wa mnyama na binadamu na kimoja kilikutwa na bangi pamoja na kete 21 za madawa ya kulevya na kingine kilikutwa na bangi pamoja na kete 18 na hivyo kufanya jumla ya kete hizo kuwa 69, alikuwa akienda nchini Uingereza na ndege ya Shirika la ndege la British Airways,” alisema Kiponza

Alisema baada ya kumhoji aliwaeleza kuwa alikuwa akiishi maeneo ya Makumbusho na Polisi walifika mpaka nyumba aliyokuwa akiishi, lakini hawakufanikiwa kukamata kitu chochote.

Alifafanua ndugu wa Halid walithibitisha kumfahamu ndugu yao ila walipoulizwa kazi anayoifanya walidai hawaifahamu na kufafanua kuwa wanachokijua ni kuwa ndugu yao anaishi nchini Uingereza.

Alipoulizwa swali na gazeti hili, njia zinazotumiwa na jeshi hilo kuwabaini watu mbalimbali wanaobeba madawa ya kulevya, Kiponza alisema; “kitu cha kwanza kinachotusaidia ni mashine zilizopo pale uwanjani, sikatai wapo wanaopita ila huwa tunakuwa makini sana hasa kwa wasafiri ambao hutoka au kwenda nchi ambazo zinasifika kwa biashara za madawa haya.”

Alisema wanatunza kumbukumbu za hati za kusafiria za wasafiri wanaokwenda katika nchi hizo na kunakili tarehe wanazoondoka na watakayorejea ili iwe rahisi kwao kuwafuatilia licha ya kuwa wakati mwingine wasafiri hao hurudi bila kuwa na mzigo wowote. Fidelis Butahe na Zaina Malongo: SOURCE:: MWANANCHI

No comments: