Monday, February 22, 2010

TCU yatambua rasmi digrii za Dk Mathayo





KAMISHENI ya vyuo vikuu nchini (TCU) imesema imevitambua na kuvithibitisha vyeti vya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk David Mathayo.

Katika barua iliyoandikwa kwenda kwa Dk Mathayo kutoka kwa Katibu mkuu wa TCU, Profesa Mayunga Nkunya, TCU imeeleza kuridhishwa kwake na uhalali wa vyeti vya shahada ya kwanza, shahada ya pili na cheti cha shahada ya falasafa (Ph.D) vilivyowasilishwa kwenye kamisheni hiyo.

“Kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa TCU chini ya kifungu 5-(1)(n) cha sheria ya vyuo vikuu namba 7 ya mwaka 2005, tunapenda kutambua uhalali wa vyeti vyako ambavyo vinakubalika kwa misingi ya vyuo vikuu,” ilieleza barua hiyo ya TCU.

Barua hiyo iliyoandikwa Februari 13, 2010 ilieleza kuwa vyeti hivyo vya taaluma ni vile vinavyoonyesha kuwa Dk David Mathayo alipata shahada yake ya kwanza ya udaktari wa mifugo katika chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (1997).

Baada ya hapo, aliweza kupata shahada ya pili ya Sayansi ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini mwaka 2001 na kupata shahada ya juu ya udaktari wa Falsafa (Ph.D) katika Sayansi ya wanyama kwenye chuo kikuu cha Free State nchini Afrika Kusini mwaka 2003.

Profesa Nkunya pia ameelekeza nakala za batrua hiyo kwa Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Katibu mkuu kiongozi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Imeandikwa na Andrew Msechu; SOURCE: MWANANCHI.

2 comments:

Anonymous said...

bado sasa dr nchimbi

Anonymous said...

HUYU MKUNYA ANA AGENDA YAKE BINAFSI HAPENDI WATU WENGINE WAONEKANA WAMESOMA NI UPUUZI MTUPU