MAREHEMU BALOZI DAUDI MWAKAWAGO.
MWANASIASA mkongwe, mwanadiplomasia na mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Tanzania, Balozi Daudi Mwakawago amefariki dunia.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa Mwakawago alifariki dunia baada ya kuugua malaria kwa siku tisa.
Kwa mujibu wa habari hizo, zilizothibitishwa na viongozi wa CCM, Mwakawago alifikwa na mauti hayo katika hospitali ya Aga Khan iliyoko jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa CCM bara Pius Msekwa, alilieleza gazeti hili jana kuwa alipata taarifa za kifo hicho jana asubuhi.
"Ni kweli Balozi Mwakawago amefariki alfajiri ya leo (jana) katika Hospitali ya Aga Khan alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa," alisema Msekwa.
Alisema walipata taarifa hizo kutoka kwa mtoto wa marehemu, Yassin Mwakawago baada ya kufika katika ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dar es Salaam na kutoa taarifa hizo.
"Taarifa za kifo cha Balozi Mwakawago tulizipata leo (jana) asubuhi baada ya mtoto wa marehemu, Yassin Mwakawago kufika ofisini na kutueleza msiba huo," alisema Msekwa.
Balozi Mwakawago atakumbukwa kama mwanasiasa na mwanadiplomasia mwandamizi aliyeshika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi. SOURCE: Mwananchi
Comments