RAIS Jakaya Kikwete amesema kuanzia mwaka ujao wa Fedha Mahakama itatengewa bajeti yake yenyewe, ili kuwa na uwezo wa kupanga na kutumia fedha yenyewe, bila kupitia Wizara ya Katiba na Sheria.
Rais Kikwete alitoa kauli hizo wakati akitoa salamu kwenye maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ishara ya mahakama kuanza mwaka mpya wa shughuli zake.
“Kuanzia mwaka ujao wa fedha Mahakama itakuwa na bajeti yake ambapo itakuwa na uwezo wa kujipangia matumizi yake yenyewe bila kupitia wizara kama ilivyokuwa awali,” alisema Kikwete.
Hatua hiyo imekuja baada ya kilio cha muda mrefu cha mhimili huo ambapo pamoja na mambo mengine ulikuwa ukipendekeza kuwa na bajeti yao, mfuko wake na kuwa na mtendaji mkuu ambaye atakuwa anasimamia shughuli za kiutawala tofauti na ilivyo sasa.
“Kuanzia mwaka ujao wa fedha Mahakama itakuwa na bajeti yake ambapo itakuwa na uwezo wa kujipangia matumizi yake yenyewe bila kupitia wizara kama ilivyokuwa awali,” alisema Kikwete.
Awali mhimili mwengine wa dola ambao ni Bunge nao kwa muda mrefu walitoa kilio chao kwa serikali wakiomba watengewe bajeti yao kisheria jambo ambalo limefanikiwa na sasa mhimili huo umekuwa ukitengewa sehemu ya bajeti yake na kuwa na mtendaji mkuu ambaye ni Katibu Mkuu wa Bunge.
Kauli hizo za Rais zimekuja wakati ambapo kumekuwepo na kilio cha muda mrefu katika mhimili huo kutaka itengewe asilimia fulani kutoka kwenye baejti ya serikali kama ilivyo kwa mhimili mwingine wa dola (Bunge) ambalo hutengewa asilimia mbili ya bajeti ya serikali.
Kauli hiyo ya Kikwete ilitanguliwa na mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na Jaji Mkuu Agustino Ramadhani pamoja na ya wadau wengine wa sekta ya sheria waliopata nafasi ya kuhutubia katika sherehe hiz akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Fredrick Werema na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS) Dk. Fauz Twaib.
“Mliyosema yote nimeyasikia na wadau wote wanaohusika wako hapa Sisi tutayafanyia kazi. Tutaweka kipaumbele stahiki katika bajeti ili muweze kuboresha miundombinu na kuongeza ajira kwa mahakimu na watumishi wengine,” alisema Rais Kikwete na kuongeza;
“Kuanzia mwaka ujao wa fedha mahakama itakuwa na mfuko wake wa fedha wakati tukiendelea na mipango ya kuiwezesha kuwa na bajeti yake ili iwe huru katika kupanga na kutekeleza majukumu yake. Tayari tumeshafanya hivyo kwa Bunge”.
Comments